Zarif: Marekani inapasa kutekeleza makubaliano ya JCPOA
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa Marekani inapasa kufanya jitihada za kutekeleza majukumu yake kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kama inavyofanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Muhammad Javad Zarif amesema kuwa wapenda vita wanadai eti wana wasiwasi kwamba Iran haiheshimu makubaliano hayo; Marekani inapasa kwa umakini kabisa na kama inavyofanya Iran, ifanye juhudi za kutekeleza makubaliano hayo."
Rais Donald Trump wa Marekani usiku wa Ijumaa ya tarehe 13 mwezi huu alitangaza kuwa, hatoidhinisha kwamba Iran imetekeleza majukumu yake kuhusu makubaliano ya JCPOA. Trump alitoa kauli hiyo bila ya kuzingatia ripoti nane za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) zinazosisitiza kuwa, Iran imeheshimu kikamilifu makubaliano hayo.
Umoja wa Ulaya na nchi nyingine duniani pia zilitangaza baada ya Rais wa Marekani kutoa matamshi hayo kuwa, zitaendelea kuyaunga mkono kikamilifu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kama ilivyokuwa huko nyuma.
Makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa kati ya Iran na kundi la 5+1 linaloundwa na Uingereza, Ufaransa, Russia, Uchina, Marekani pamoja na Ujerumani yalianza kutekelezwa Januari mwaka jana. Hata hivyo serikali ya Marekani ikiwa moja ya nchi wanachama wa kundi hilo, imekuwa ikikwepa kutekeleza makubaliano hayo.