Iran itaendelea kushirikiana na IAEA, kufungamana na JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i36041
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema kuna haja Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) uendelee kuwa chombo huru na kisichoegemea upande wowote akisisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na wakala huo.
(last modified 2025-07-22T07:00:06+00:00 )
Oct 30, 2017 08:00 UTC
  • Iran itaendelea kushirikiana na IAEA, kufungamana na JCPOA

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema kuna haja Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) uendelee kuwa chombo huru na kisichoegemea upande wowote akisisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na wakala huo.

Rais Rouhani alisema hayo jana Jumapili katika mkutano wake na Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Yukia Amano, ambaye yuko hapa Tehran kwa ziara rasmi ya kikazi.

Dakta Rouhani amebainisha kuwa: "Kutokana na ukweli kwamba Iran imeonyesha ushirikiano mkubwa na IAEA katika miaka ya hivi karibuni, wakala huo unapaswa kutoa ripoti yake ya mwisho kuhusu miradi ya nyuklia yenye malengo ya amani ya taifa hili."

Rais wa Iran ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kufungamana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, maadamu taifa hili litaendelea kustafidi na mwafaka huo.

Rais Rouhani na Yukia Amano

Hapo jana Amano alisema kuwa Iran imefungamana na kutekeleza wajibu na majukumu yake kuhusu makubaliano ya nyuklia maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). 

Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki hadi kufikia sasa umethibitisha mara nane kwamba Iran imeheshimu na kufungamana kikamilifu na makubaliano hayo ya nyuklia; huku Marekani iking'ang'ania kuwa Iran imekwenda kinyume na makubaliano hayo licha ya wakala wa IAEA kukagua mara kwa mara vituo vya nyuklia hapa nchini.