Iran yakadhibisha 'madai ya kitoto' ya Bahrain kuhusu kushambuliwa bomba la mafuta
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i36359-iran_yakadhibisha_'madai_ya_kitoto'_ya_bahrain_kuhusu_kushambuliwa_bomba_la_mafuta
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha kile ilichokitaja kama 'madai ya kitoto' yaliyotolewa na Bahrain dhidi yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 13, 2017 00:49 UTC
  • Iran yakadhibisha 'madai ya kitoto' ya Bahrain kuhusu kushambuliwa bomba la mafuta

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha kile ilichokitaja kama 'madai ya kitoto' yaliyotolewa na Bahrain dhidi yake.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bahram Qassemi amesema tuhuma za Bahrain kwamba Iran ilihusika katika mripuko uliotokea usiku wa kuamkia Jumamosi katika bomba la kusafirishia mafuta kusini mwa mji mkuu Manama ni 'njozi' na madai yasiyo na msingi.

Qassemi amesema kile ambacho watawala wa Manama wamefunzwa na mabawana wao kutamka baada ya ajali hiyo ni kuinyooshea kidole cha lawama Iran.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameukumbusha utawala wa Aal-Khalifa wa Bahrain kwamba, zama za kuibuka na kutoa madai ya kinjozi, urongo na tuhuma za kitoto zimepitwa na wakati.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bahram Qassemi

Bomba hilo la kusafirishia mafuta kati ya Saudi Arabia na Bahrain linalomilikiwa na shirika la mafuta la Bahrain (Bapco) liliripuka Ijumaa usiku, na kusababisha moto mkubwa kusambaa katika kijiji cha Buri, viungani mwa mji mkuu Manama.

Katika hali ambayo hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa katika tukio hilo, wala kundi lolote kutangaza kuhusika na mripuko huo, lakini Khalid bin Ahmed Aal-Khalifah, Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain alidai kuwa yumkini kuna mkono wa Iran kwenye tukio hilo.