Iran: Sumu hatari ya Uwahabi na Utakfiri ilizaliwa Saudi Arabia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i36476-iran_sumu_hatari_ya_uwahabi_na_utakfiri_ilizaliwa_saudi_arabia
Mshauri na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Saudi Arabia ndio chimbuko na sehemu ilikozaliwa idiolojia hatari ya Utakfiri inayotumiwa na magenge ya kigaidi kama vile Daesh (ISIS).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 18, 2017 04:22 UTC
  • Iran: Sumu hatari ya Uwahabi na Utakfiri ilizaliwa Saudi Arabia

Mshauri na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Saudi Arabia ndio chimbuko na sehemu ilikozaliwa idiolojia hatari ya Utakfiri inayotumiwa na magenge ya kigaidi kama vile Daesh (ISIS).

Mohammad Hassani-Nejad aliyasema hayo jana Ijumaa na kufafanua kuwa, sumu hatari ya Utakfiri iliyozaliwa Saudia ni jinamizi lisiloweza kufumbiwa macho hata kidogo.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran amebainisha kuwa: "Idiolojia ya Utakfiri ni jinamizi linalotaka kutafuna na kumaliza viumbe vyote duniani."

Uwahabi, pembe ya shetani

Mshauri na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, serikali ya Riyadh, mashirika ya utoaji misaada ya Saudia na waungaji mkono wao wanaendelea kuunga mkono utakfiri, chombo kinachohitajika ili kufanikisha na kueneza harakati za kigaidi na misimamo ya kufurutu ada.

Matamshi ya Hassani-Nejad ni radiamali ya Iran kwa tuhuma zilizotolewa na Abdallah al-Mouallimi, Balozi wa Saudia katika Umoja wa Mataifa, aliyedai kuwa Jamhuri ya Kiislamu inatumia migawanyiko ya kimadhehebu katika nchi za Iraq, Lebanon na Syria kwa ajili ya maslahi yake ya kisiasa.