Zarif: Ni maskhara kuona Saudi Arabia ikiituhumu Iran kuwa inasababisha machafuko
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa ni maskhara kwa Saudia Arabia kuituhumu Iran kuwa inasababisha machafuko katika hali ambayo nchi hiyo ndiyo inayowachochea magaidi na iliyoanzisha vita huko Yemen.
Muhammad Javad Zarif amesema kuwa ni maskhara kuona kuwa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia unaituhumu Iran kuwa inavuruga amani katika hali ambayo wenyewe ndiyo unaowakusanya magaidi na iliyoanzisha vita huko Yemen na umeizingira Qatar na kuchochea mgogoro wa ndani huko Lebanon.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria pia kikao cha pande tatu cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Uturuki na Russia huko Antaliya, Uturuki na kueleza kuwa nchi hizo tatu zinashirikiana ili kupanua usitishaji vita huko Syria. Zarif ameongeza kuwa, nchi hizo tatu zinajitayarisha kwa ajili ya mazungumzo mapana kati ya makundi ya Wasyria.
Kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje nchi za Iran, Russia na Uturuki zinazosimamia makubaliano ya usitishaji vita Syria kilifanyika jana Jumapili katika mji wa Antaliya Uturuki kwa ajili ya kushauriana kuhusu mgogoro wa Syria.