Tehran mwenyeji wa Kongamano la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu
Duru ya 31 ya Kongamano la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu imeng'oa nanga hii leo hapa katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Tehran.
Kongamano hilo linawashirikisha shakhsia zaidi ya 500 kutoka nchi mbali mbali duniani, wakiwemo mawaziri, wanavyuoni, maprofesa wa vyuo vikuu na wajumbe kutoka jumuiya za kimataifa za sayansi na utamaduni.
Kongamano hilo la siku tatu limefunguliwa kwa hotuba ya Hassan Rouhani wa Iran.
Pambizoni mwa kongamano hilo, kutafanyika pia mkutano wa Umoja wa Kimataifa wa Wanawake Waislamu na Jumuiya ya Kimataifa ya Wanavyuoni Wanamuqawama.

Washirika wa kongamano hilo hapo kesho Jumatano watapa fursa ya kukutana na Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Hapo jana, washiriki wa kongamano walizuru Haram ya Imam Rouhullah Khomeini, Mwasisi na Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kongamano la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu linafanyika wakati huu ambapo dunia inaadhimisha Wiki ya Umoja wa Kiislamu.

Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni kipindi cha kati ya tarehe 12 na 17 za Mfunguo Sita Rabiu Awwal, kipindi ambacho kinasadifiana na kuadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume SAW.
Wiki ya Umoja wa Kiislamu ilizaliwa kutokana na ubunifu wa Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini (MA).