Iran yamuita balozi wa Uswisi kulalamikia madai bandia ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i37833-iran_yamuita_balozi_wa_uswisi_kulalamikia_madai_bandia_ya_marekani
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemuita balozi wa Uswisi mjini Tehran na kumkabidhi malalamiko rasmi kufuatia madai ya hivi karibuni ya Marekani kwamba makombora yanayofyatuliwa na vikosi vya Yemen dhidi ya Saudia yametoka Iran.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 20, 2017 02:38 UTC
  • Iran yamuita balozi wa Uswisi kulalamikia madai bandia ya Marekani

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemuita balozi wa Uswisi mjini Tehran na kumkabidhi malalamiko rasmi kufuatia madai ya hivi karibuni ya Marekani kwamba makombora yanayofyatuliwa na vikosi vya Yemen dhidi ya Saudia yametoka Iran.

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema balozi huyo wa Uswisi ambaye ofisi yake inashughulikia maslahi ya Marekani mjini Tehran amekabidhiwa barua hiyo ya kulalamikia madai yasiyo na msingi, ya kichochezi na yasiyo ya uwajibikaji ya Marekani dhidi ya nchi hii.

Si vibaya kukumbusha kuwa, Washington haina ubalozi hapa Iran tangu mwaka 1980, na ubalozi wa Uswisi mjini Tehran umekuwa ukishughulikia maslahi ya Marekani hapa nchini.

Haley akiwa nyuma ya mabaki ya makombora anayodai yametoka Iran

Alkhamisi iliyopita, Nikki Haley, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa aliituhumu Iran kuwa eti inaizatiti kwa makombora ya balestiki harakati ya Ansarullah ya Yemen kwa ajili ya kuishambulia Saudia.

Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq ameyakanusha madai hayo yaliyotolewa na mwakilishi huyo wa Marekani katika umoja huo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu itayawasilisha kwa Umoja wa Mataifa madai ya Nikki Haley, kwamba eti Iran imeipatia silaha harakati ya Ansarullah ya Yemen.