Irada ya Iran ya kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i38329-irada_ya_iran_ya_kuimarisha_uhusiano_na_nchi_za_afrika
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitza azma yake ya kuimarisha uhusiano na nchi za bara la Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 31, 2017 04:19 UTC
  • Irada ya Iran ya kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitza azma yake ya kuimarisha uhusiano na nchi za bara la Afrika.

Hayo yalisemwa Jumamosi mjini Tehran katika Kikao cha Idara Maalumu ya Uhusiano na Bara la Afrika ya Serikali ya Iran. Mwenyekiti wa idara hiyo ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran Bw. Ishaq Jahangiri  ameashiria azma na irada imara ya Iran ya kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika na kusema, "kuinua kiwango cha uhusiano na nchi za Afrika katika sekta za kisiasa na kiuchumi ni jambo lenye umuhimu mkubwa kwa Iran."

Jahangiri ametaka kuchukuliwe hatua za kuimarisha mabadilishano ya kiuchumi na kwa msingi huo ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran iandae mikakati ya kuboresha zaidi uhusiano na nchi za Kiafrika. Hali kadhalika ametoa wito kwa sekta binafsi nchini ishiriki zaidi katika miradi ya maendeleo na uwekezaji barani Afrika.

Rais Zuma  wa Afrika Kusini (kushoto) na Rais Rouhani wa Iran Aprili 2016

Kikao hicho kilihudhuriwa na mawaziri wa mambo ya nje, kilimo, biashara, ushirika pamoja na wawakilishi wa sekta binafsi.

Katika kikao hicho cha Idara Maalumu ya Uhusiano na Bara la Afrika ya Serikali ya Iran, washiriki walijadili pia njia za kuimarisha uhusiano wa kibenki na kurahisisha biashara pamoja na kupunguza gharama za uchukuzi ili kuboresha mabadilishano ya kibiashara ya Iran na nchi za Afrika.

Aidha serikali ya Iran imesema itatenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara na wawekezaji wa Iran wanaoshiriki katika miradi mbali mbali barani Afrika.