Zarif amjibu Trump, asema hakuna mazungumzo kuhusu mapatano ya nyuklia ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i38901-zarif_amjibu_trump_asema_hakuna_mazungumzo_kuhusu_mapatano_ya_nyuklia_ya_iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu matamshi ya kujitakia makuu ya Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na kusema haiwezekani kufanya mazungumzo mapya kuhusu mapatanao hayo huku akiitaka Marekani itekeleze ahadi zake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 13, 2018 01:18 UTC
  • Zarif amjibu Trump, asema hakuna mazungumzo kuhusu mapatano ya nyuklia ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu matamshi ya kujitakia makuu ya Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na kusema haiwezekani kufanya mazungumzo mapya kuhusu mapatanao hayo huku akiitaka Marekani itekeleze ahadi zake.

Katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twitter Ijumaa usiku, Zarif  amesema sera za Trump na taarifa yake siku ya Ijumaa ni katika jitihada za mwisho zitakazofeli za kutaka kuvuruga mapatano imara ya pande kadhaa ambayo yameidhinishwa na Umoja wa Mataifa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.

Zarif ameendelea kusema kuwa, mapatano ya JCPOA hayawezi kufanyiwa mazungumzo tena na ni kwa sababu hii ndio badala ya Marekani kukariri maneno yaliyochakaa, inapaswa, kama Iran, kufungamana na mapatano hayo.

Siku ya Ijumaa, Rais Donald Trump wa Marekani kwa mara nyingine alirefusha muda wa kusitisha vikwazo vya nyuklia vya Iran licha ya kutoridhishwa na makubaliano hayo. Aidha katika hatua nyingine ya uhasama Trump alitangaza kuweka vikwazo visivyo vya nyuklia dhidi ya Iran ambavyo vimelenga watu na taasisi 14.

Kwa mujibu wa sheria ya ndani ya Marekani, Rais wa nchi hiyo anapasa kuwasilisha ripoti kwa Kongresi ya nchi hiyo kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mara moja kila baada ya siku 90. 

Rais Trump

Trump amesema iwapo mazungumzo mapya hayatafanyika kuhusu mapatano ya JCPOA basi hatayaidhinisha baada ya miezi mitatu ijayo. Mtawala huyo wa Marekani anataka kadhia ya makobora ya kuijihami ya Iran iingizwe katika mapatano hayo ya nyuklia jambo ambalo Iran imelipinga vikali. 

Ikumbukwe kuwa Iran na kundi la nchi za 5+1 ambazo ni Russia, China, Ufaransa, Uingereza, Marekani na Ujerumani zilitiliana saini mapatano ya nyuklia Julai 14, 2015 baada ya miaka miwili na nusu ya mazungumzo ya kina ya nyuklia.

Kwa mujibu wa mapatano hayo yaliyoanza kutekelezwa Januari 16 mwaka huu, vikwazo vyote vilivyohusiana na miradi ya nyuklia vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya, Marekani na Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vilipaswa kuondolewa.

Mkabala wa hilo Iran ilitakiwa kupunguza baadhi ya shuguhuli zake za nyuklia. Iran imeshatekeleza ahadi zake lakini nchi za Ulaya na Marekani bado hazijatekeleza ahadi zilizotoa.