Rais Rouhani: Serikali inalenga kuharakisha utekelezaji wa Uchumi wa Muqawama
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema azma ya serikali ni kuharakisha mwenendo wa utekelezaji Uchumi wa Muqawama.
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo katika mkutano na wakuu na watendaji wa vyombo mbalimbali vya serikali na kutangaza kuwa katika mwaka huu mpya wa 1395 Hijria Shamsia, ambao Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameupa jina la Mwaka wa "Uchumi wa Muqawama; Hatua na Utekelezaji", serikali imedhamiria kuendeleza na kuzipa msukumo wa kasi zaidi fursa zilizojitokeza baada ya kuondolewa vikwazo ili kufanikisha utekelezaji wa sera zilizotangazwa za Uchumi wa Muqawama.
Rais Rouhani amesema kutoa msukumo kwa uzalishaji wa ndani, kuandaa mipango ya kustawisha uchumi katika sekta zote, kuandaa ajira kwa vijana, kujenga maelewano chanya na dunia na kuvutia uwekezaji na teknolojia na miongoni mwa nukta zilizotiliwa mkazo katika sera za Uchumi wa Muqawama.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa kwa mwongozo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na umoja baina ya viongozi na wananchi kadhia ya nyuklia na vikwazo vya kidhalimu dhidi ya taifa la Iran vimehatimishwa; na akaongezea kwa kusema shughuli za nyuklia zimekuwa ni alama na nembo ya ushirikiano baina ya dunia na Iran na kwamba huo ulikuwa ni ushindi mkubwa kwa taifa la Iran katika mwaka uliopita.../