Senegal yapongeza uungaji mkono wa Iran kwa Waislamu duniani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i39541-senegal_yapongeza_uungaji_mkono_wa_iran_kwa_waislamu_duniani
Balozi wa Senegal nchini Iran amepongeza uungaji mkono na mchango wa Jamhuri ya Kiislamu kwa Waislamu kote duniani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 27, 2018 07:55 UTC
  • Senegal yapongeza uungaji mkono wa Iran kwa Waislamu duniani

Balozi wa Senegal nchini Iran amepongeza uungaji mkono na mchango wa Jamhuri ya Kiislamu kwa Waislamu kote duniani.

Babakr Baa ameyasema hayo katika mkutano wake na maafisa wa ngazi za juu wa mji wa Maybod, katika mkoa wa kati wa Yazd.

Balozi huyo wa Senegal mjini Tehran amebainisha kuwa, msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuunga mkono ulimwengu wa Kiislamu ni jambo la kupigiwa mfano.

Kadhalika amesisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano na ushirikiano wa pande mbili kati ya Tehran na Dakar katika nyuga mbali mbali. 

Katika mazungumzo na Gavana wa mji wa Maybod, Hossein Fallah, mwanadiplomasia huyo wa Senegal amesema Dakar inaridhishwa na kiwango cha sasa cha uhusiano na ushirikiano wa nchi yake na Iran na inatoa wito kuimarishwa zaidi uhusiano huo.

Rais Rouhani na ujumbe wa Senegal ukiongozwa na Spika wa nchi hiyo ya Afrika mjini Tehran siku chache zilizopita

Aliyasema hayo baada ya kusaini hati ya makubaliano ya kumarisha uhusiano wa vyuo vikuu vya nchi mbili hizi na kubainisha kuwa, Tehran na Dakar zinaweza kutumia fursa zilizopo kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika nyuga za utamaduni, sayansi na viwanda.

Kwa upande wake, Gavana wa mji wa Maybod, Hossein Fallah amepongeza mapambano ya nchi za Afrika ikiwemo Senegal dhidi ya ukaliaji wa mabavu wa ardhi zao zama za ukoloni.

Amesema mji wa Meybod ni mzalishaji mkubwa wa vigae na seramiki ambapo umekuwa ukiziuza katika nchi za Pakistan, Afghanistan, Imarati na Oman miongoni mwa nchi nyingine, na kwamba suala la kuanza kuuza bidhaa hizo kwa nchi za Afrika lipo katika ajenda.