Iran: Ushirikiano wa kimataifa unahitajika kuangamiza zimwi la ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i39587-iran_ushirikiano_wa_kimataifa_unahitajika_kuangamiza_zimwi_la_ugaidi
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani shambulizi la kigaidi lilioutikisa mji mkuu wa Afghanistan, Kabul hapo jana na kuua makumi ya watu na kujeruhi wengine wengi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 28, 2018 04:32 UTC
  • Iran: Ushirikiano wa kimataifa unahitajika kuangamiza zimwi la ugaidi

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani shambulizi la kigaidi lilioutikisa mji mkuu wa Afghanistan, Kabul hapo jana na kuua makumi ya watu na kujeruhi wengine wengi.

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema jinamizi la ugaidi haliwezi kutokomezwa pasina ushirikiano na jitihada za pamoja za nchi za eneo na dunia nzima kwa ujumla.

Amesema, "kuukabili ugaidi kunahitaji ushirikiano wa dhati na juhudi zisizo na kikomo za nchi za eneo hili la Mashariki ya Kati na dunia nzima kwa ujumla."

Huku hayo yakirifiwa, idadi ya watu waliopoteza maisha katika shambulizi hilo la jana imeongezeka na kupindukia 95, huku wengine zaidi ya 200 wakijeruhiwa.

Gari la kubeba wagonjwa lililotegwa bomu Kabul

Hapo jana mripuko wa bomu la kutegwa ndani ya ambulensi ulitokea karibu na ofisi za balozi za nchi kadhaa na majengo ya serikali katikati ya Kabul, mji mkuu wa nchi hiyo.

Mtandao wa kigaidi wa Taliban umekiri kuhusika na shambulizi hilo, wiki moja baada ya kutekeleza hujuma nyingine iliyoua watu zaidi ya 20 katika Hoteli ya Intercontinental mjini Kabul.