Mapinduzi ya Kiislamu; uungaji mkono kwa mapambao ya Kiislamu na Quds Tukufu
Hii leo ulimwengu wa Kiislamu ungali una madonda makongwe ambayo yamesababishwa na madola ya kiistikbari kwa Umma wa Kiislamu na muhimu zaidi kati ya madonda hayo ni suala la Palestina na kuendelea siasa za utawala haramu wa Israel za kughusubu ardhi za Waislamu.
Mrengo wa kufri, uistikbari na uzayuni umekuwepo kwa zaidi ya miaka 70 sasa ambapo umeteka ardhi za Palestina na kuzifanya kuwa kituo cha kuvuruga usalama wa nchi za Mashariki ya Kati na kubuni kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh kwa ajili ya kukamilisha njama za kuvuruga hali ya mambo katika eneo. Hii leo ulimwengu wa Kiislamu unaweza kusimama imara mbele ya kufri na uistikbari na mfumo wa Kiislamu nchini Iran ambao unafuatilia kutekelezwa kikamilifu sheria za Kiislamu, utakuwa njia ya ushindi dhidi ya maadui wa Uislamu. Akizungumza katika kikao cha wageni walioshiriki katika kongamano la Wanaowapenda Ahlul Beit (as) na Suala la Wakufurishaji, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza juu ya kusimama imara huko na kusema: 'Licha ya kuwepo mashinikizo haya yote, tunatangaza wazi kwamba Jamhuri ya Kiislamu itatoa msaada wake katika kila sehemu ambayo msaada huo unahitajika kwa ajili ya kupambana na kufri na uistikbari, na wala hatutamjali yoyote katika hilo.'
Matamshi hayo ya Kiongozi Muadhamu yana nukta muhimu mno na sifa maalumu ambazo haziwezi kutiwa doa kuhusiana na mapambano ya taifa la Iran dhidi ya uistikbari, mapambano ambayo yana mizizi katika Mapinduzi ya Kiislamu na ukakamavu mbele ya mifumo ya kibeberu. Huku akisistiza kuwa nchini Iran jeshi limeimarishwa na kuwa na nguvu kubwa, Meja Jenerali Muhammad Baqeri, Kamanda Mkuu wa Majeshi ya Iran amesisitiza kuwa majeshi hayo yana majukumu muhimu mbele ya vitisho na kulinda usalama wa mipaka ya nchi hii. Amesema Iran iko katika mstari wa mbele wa kuwakomboa wananchi wa eneo kutoka makucha ya uistikbari na kwamba Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yanakwenda kwa kasi kubwa kuelekea malengo yake matukufu.
Hii leo fitina ya Daesh imewaondokea watu wa magharibi mwa Asia lakini pamoja na hayo bado kitovu cha fitina hiyo, yaani jipu la saratani la utawala haramu wa Israel, kingalipo. Ni kwa kutilia maanani nukta hiyo muhimu ndipo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akasisistiza: 'Siku ambayo Palestina itawarejea Wapalestina, hilo litakuwa ni pigo kubwa na la uhakika kwa uistikbari na sisi tutaendelea kufanya juhudi za kufikia siku hiyo.'
Akizungumza mbele ya wageni walioshiriki katika kikao cha 13 cha kimataifa cha Mabunge ya Nchi za Kiislamu hapa mjinji Tehran, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kuwa kutetea Palestina ni jukumu la wote na kusisitiza kwamba hatupasi kudhani kwamba mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni hayana faida yoyote bali kwa uwezo wake Mungu, juhudi hizi zote za kukabiliana na utawala huo zitakuwa na matokeo ya kuridhisha. Kama ambavyo tunaona kwamba mrengo wa mapambano ya Kiislamu umepata mafanikio makubwa katika miaka iliyopita.
Uzingatiaji na masisitizo ya mara kwa mara ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusiana na suala la Palestina ni jambo lililomvutia sana mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakata ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, kiasi cha kumfanya amwandikie barua Kiongozi wa Mapinduzi hivi karibuni akimsifu na kumshukuru kutokana na misimamo yake imara kuhusiana na suala zima la Palestina. Katika barua hiyo, Ismail Hania alisema kuwa watu wote shupavu wa Palestina wanatambua vyema msimamo imara na wenye thamani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na suala la Palestina, Quds Tukufu na uungaji mkono wa Iran kwa mapambano ya watu wa Palestina kupitia misaada yake tofauti kwao.
Katika fikra ya kimapinduzi na ya kupigania uhuru ya Imam Khomeini (MA), suala la kukombolewa Palestina ni msingi usioweza kutiwa doa. Anawaarifisha Wazayuni kwa kusema: 'Israel ilibuniwa na serikali za kikoloni za Magharibi na Mashariki kwa ajili ya kukandamiza mataifa ya Kiislamu na leo inaungwa mkono na wakoloni wote.' Uingereza na Marekani zinauimarisha utawala ghasibu wa Israel kwa njia tofauti zikiwemo za kisiasa, kiuchumi na kijeshi na kuupa silaha hatari kwa ajili ya kuchokoza na kizivamia nchi za Kiarabu na Kiislamu. Hayati Imam Khomeini (MA) daima alikuwa akisisitiza kwamba uchokozi na ukaliwaji mabavu wa ardhi za Palestina, Lebanon na miinuko ya Golan nchini Syria unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel hauwezi kukomeshwa kupitia mapatano eti ya amani na utawala huo, bali utawala huo na washirika wake wanaendelea kufuatilia ndoto ya kubuniwa Israel kubwa katika eneo, na hatari ya jambo hilo kuzikabili nchi zote za Mashariki ya Kati na ardhi za Waislamu.