Velayati: Muqawama utawatimua Marekani, Wazayuni Euphrates Mashariki
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i40493-velayati_muqawama_utawatimua_marekani_wazayuni_euphrates_mashariki
Afisa wa ngazi za juu nchini Iran amesema harakati ya muqawama katika eneo itaitimua Marekani na utawala haramu wa Kizayuni kutoka eneo la Mashariki mwa Mto Euphrates ambao unatiririka kutoka Uturuki na kupitia Syria hadi Iraq.
(last modified 2025-12-03T16:38:35+00:00 )
Feb 17, 2018 17:11 UTC
  • Velayati: Muqawama utawatimua Marekani, Wazayuni Euphrates Mashariki

Afisa wa ngazi za juu nchini Iran amesema harakati ya muqawama katika eneo itaitimua Marekani na utawala haramu wa Kizayuni kutoka eneo la Mashariki mwa Mto Euphrates ambao unatiririka kutoka Uturuki na kupitia Syria hadi Iraq.

Ali Akbar Velayati, mshauri wa ngazi za juu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatollah Sayyed Ali Khamenei ametoa tamko hilo katika kongamano la Umoja wa Kiislamu ambalo limefanyika katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad hii leo.

Velayati amesema Wamarekani na baadhi ya Waarabu wanajaribu 'kuunda Mashariki ya Kati mpya ambayo msingi wake ni kuvuruga jamii za Waislamu."

Velayati amesema Marekani inalenga kuigawa Syria na inafanya hivyo kupitia vikosi vyake mashariki mwa Euphrates.

Aidha ameashiria safari ya hivi karibuni Mashariki ya Kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson na kusema safari hiyo imelenga kuzidisha mgawanyiko katika Umma wa Waislamu na nchi za Waislamu.

Velayati amesema Marekani inataka kuongeza  vituo vya Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO kwa msaada wa baadhi ya nchi za Waislamu ili kuhakikisha kuwa haziungani.

Wanajeshi wa Marekani nchini Syria

Aidha amesema: "Wamarekani na Wazayuni wafahamu kuwa walishindwa Lebanon, Syria na Iraq na hivyo ndoto zao hazitafanikiwa." Ameongeza kuwa harakati za mapambano ya Kiislamu huko Iraq, Syria na Lebanon zitawatimua Wamarekanin na Wazayuni kutoka eneo la mashariki mwa Mto Euphrates.

Eneo la kaskazini mashariki mwa Syria lililoko upande wa Euphrates mashariki linadhibitiwa na wanamgambo wa  Kikurdi wa SDF-YPG ambao wanaungwa mkono na Marekani.