Iran na Uhispania zasisitiza kupanua zaidi ushirikiano baina yao
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i40697-iran_na_uhispania_zasisitiza_kupanua_zaidi_ushirikiano_baina_yao
Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uhispania wamesisitiza azma ya nchi zao ya kustawisha zaidi uhusiano na ushirikiano baina yao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 22, 2018 00:58 UTC
  • Iran na Uhispania zasisitiza kupanua zaidi ushirikiano baina yao

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uhispania wamesisitiza azma ya nchi zao ya kustawisha zaidi uhusiano na ushirikiano baina yao.

Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na Alfonso Dastis, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uhispania walisisitiza hayo jana katika mazungumzo yao hapa mjini Tehran na kueleza kwamba, Tehran na Madrid zimeazimia kwa dhati kustawisha zaidi uhusiano na ushirikiano katika nyanja za utalii, mazingira, nishati, teknolojia ya kisasa, elimu na usafiri na uchukuzi.

Dakta Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameashiria katika mazungumzo husiano mkongwe wa pande mbili na kusema kuwa, ni jambo la dharura kwa pande mbili kustawisha uhusiano katika nyuga zote.

Mazungumzo ya Rais Rouhani na Alfonso Dastis, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uhispania

Kwa upande wake, Alfonso Dastis, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uhispania amesema katika mazungumzo na mwenyeji wake kwamba, amefurahishwa na safari yake hapa Tehran na kwamba ni kwa mara ya kwanza anaitembelea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Alfonso Dastis, sambamba na kusisitiza udharura wa kutekelezwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ameeleza kwamba, Uhispania ikiwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, inafungamana kikamilifu na makubaliano hayo.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uhispania aliwasili hapa Tehran Jumanne usiku kwa safari rasmi ya kikazi ambapo mbali na Zarif, ameshakutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Tehran akiwemo Rais Hassan Rouhani.