Iran: Tutajiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia iwapo hayatakuwa na maslahi kwetu
Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran itajiondoa mara moja kwenye makubaliano ya nyuklia iwapo itahisi mapatano hayo hayana maslahi kwa taifa hili.
Mohammad Baqer Nobakht hata hivyo amesisitiza kuwa, Iran kwa sasa itaendelea kutekeleza wajibu wake juu ya makubaliano hayo, yanayojulikana kama JCPOA.
Amesema, "Iwapo tutahisi maslahi yetu hayajafikiwa kwenye makubaliano hayo, basi hatutasalia kwayo hata sekunde moja."
Msemaji wa serikali ya Iran ameongeza kuwa, msimamo alioutoa kuhusu JCPOA sio wake binafsi bali ni jambo ambalo limejikita kwenye Mfumo wa Kiislamu wa nchi hii.
Licha ya Iran kufungamana na makubaliano hayo tangu yapasishwe Julai 2015, lakini Marekani imekuwa ikiamiliana na Tehran kwa vitisho na vikwazo na kukwepa kutekeleza majukumu yake.
Makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na nchi sita za Russia, Ufaransa, Uingereza, China, Marekani na Ujerumani yalianza kutekelezwa Januari mwaka 2016.