Boroujerdi: Iran haitoheshimu maafikiano ya JCPOA iwapo itahisi hayana faida kwake
Mkuu wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Siasa za Kigeni ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesisitiza kuwa, Tehran inaendelea kuheshimu maafikiano ya nyuklia ya JCPOA kutokana na kuhisi ina manufaa ndani yake, lakini kama Marekani itajitoa kwenye maafikiano hayo, Iran nayo haitaona haja ya kuendelea nayo.
Shirika la habari la IRIB limemnukuu Alaeddin Boroujerdi akisema hayo kujibu madai ya Nikki Haley, mwakilishi wa kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa aliyedai kuwa Iran haiwezi kujitoa katika maafikiano hayo iwapo Marekani itajitoa kutokana na uhusiano wa kibiashara uliopo baina ya Tehran na Umoja wa Ulaya. Boroujerdi amesema: Nikki Haley hawezi kuipangia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nini cha kufanya.
Amesema, viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamesema mara kadhaa kwamba wanachukua maamuzi yao kwa kuangalia maslahi ya taifa na iwapo kutoka Marekani katika maafikiano ya nyuklia ya JCPOA kutapelekea kuongezeka vikwazo dhidi yake, bila ya shaka yoyote Iran nayo haitobakia kwenye maafikiano hayo.
Amesema uhusiano wa Iran na Umoja wa Ulaya ni wa jadi na ni wa muda mrefu na kuongeza kuwa, uhusiano huo utaendelea kuwepo madhali utaendelea kuchunga misingi ya kuheshimiana na wala hautegemei kuwepo au kutokuwepo maafikiano ya nyuklia ya JCPOA.
Maafikiano ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1 linaloundwa na nchi za Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Marekani na Ujerumani yalianza kutekelezwa mwezi Januari 2016, hata hivyo serikali ya Marekani ambayo ni moja ya nchi zilizoshiriki kikamilifu katika kufikiwa maafikiano hayo, imekuwa muda wote ikikanyaga vipengee vya JCPOA na hivi sasa ina nia ya kujitoa.