Iran na Senegal zaazimia kuimarisha uhusiano baina yao
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i42898-iran_na_senegal_zaazimia_kuimarisha_uhusiano_baina_yao
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Senegal zimesisitiza juu ya azma ziliyonayo ya kuimarisha zaidi ushirikiano baina yao zikiwa nchi mbili wanachama katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 10, 2018 02:50 UTC
  • Iran na Senegal zaazimia kuimarisha uhusiano baina yao

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Senegal zimesisitiza juu ya azma ziliyonayo ya kuimarisha zaidi ushirikiano baina yao zikiwa nchi mbili wanachama katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC.

Hayo yalisisitizwa jana mjini Dakar katika mazungumzo kati ya Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Moustapha Niasse, Spika wa Bunge la Senegal ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Muungano wa Mabunge ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC.

Dakta Zarif ambaye aliwasili Dark Senegal jana Jumatatu ikiwa ni kituo chake cha kwanza katika safari yake ya kiduru ambapo anazitembelea pia nchi za Namibia, Brazil na Uruguay amesema katika mazungumzo yake na Spika Moustapha Niasse kwamba, Iran imeazimia kustawisha zaidi ushirikiano wake na nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran

Aidha matukio ya kieneo, Afrika na ulimwenguni kwa ujumla pamoja na uhusiano wa nchi wanachama katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC ni miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa na viongozi hao.

Baadaye Dakta Zarif alishiriki katika mkutano wa pamoja wa kiuchumi wa Iran na Senegal na kusema kuwa, nchi mbili hizo muhimu za magharibi mwa Asia na magharibi mwa Afrika na katika ulimwengu wa Kiislamu zinaweza kuwa na taathira chanya katika kustawi uchumi wa eneo sambamba na kueneza amani na usalama kieneo na kimataifa bila kusahau kuleta uelewano na mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu.

Aidha amebainisha azma ya nchi hizo ya kuimarisha zaidi ushirikiano wao wa kiviwanda hasa katika sekta ya utengenezaji magari.