Mogherini: Kulindwa makubaliano ya nyuklia ya Iran ni muhimu kwa EU
Umoja wa Ulaya umekariri azma yake kubwa ya kutekeleza kikamilifu na pande zote makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 na kuongeza kuwa, kulindwa makubaliano hayo ni jambo lenye umuhimu.
Akizungumza jana mbele ya waandishi wa habari kabla ya kuanza mkutano wa Baraza la Masuala ya Kigeni la Umoja wa Ulaya huko Luxembourg, Mkuu wa Siasa za Nje wa umoja huo Federica Mogherini alisema kuwa, nchi za Ulaya zimetangaza wazi kwamba kulindwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni jambo lenye umuhimu. Aliongeza kuwa ni kwa maslahi ya kistratejia ya Umoja wa Ulaya kulindwa makubaliano ya JCPOA.
Kwa upande wake Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akiyakosoa makubaliano hayo yanayojulikana kwa jina rasmi la Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) yaliyofikiwa kati ya Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaani Marekani, Ufaransa, Uingereza, Uchina, Russia pamoja na Ujerumani.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari jana Jumatatu, Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya kwa mara nyingine tena alithibitisha kwamba Iran imeheshimu na kutekeleza kikamilifu majukumu yake kwa mujibu wa makubaliano hayo ya nyuklia na kuongeza kuwa, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) pia umethibisha ukweli huo kama ilivyoelezwa katika ripoti kumi za wakala huo.