Zarif: Iran haitofanya mazungumzo yoyote kuhusu JCPOA na mapatano hayo hayataongezwa chochote
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika ujumbe alioutoa jana kwa njia ya video kwamba Tehran haitofanya mazungumzo yoyote mapya kuhusu JCPOA na wala mapatano hayo ya nyuklia hayataongezwa chochote. Amesema mapatano hayo yana njia moja tu nayo ni Marekani kuheshimu vipengee vyake vyote.
Katika mkanda huo wa video, Mohammad Javad Zarif, amegusia namna Marekani inavyoendelea kukanyaga vipengee vya mapatano hayo na kusema kuwa, kama Washington itaendelea kuyapuuza mapatano ya JCPOA au kuamua kujitoa, basi Iran nayo itakuwa na haki ya kujibu jambo hilo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amesema, makelele na vitisho havitaifanya marekani ipate mapatano mapya hususan wakati huu ambapo Washington imekuwa ikiyapuuza na kuyakanyaga waziwazi mapatano yaliyopo.
Zarif ameashiria pia suala la kukaribia muda wa Marekani kuchukua maamuzi kuhusu kuendelea kusimamisha vikwazo dhidi ya Iran na kuheshimu ahadi zake katika mapatano ya JCPOA na kuongeza kuwa: Iran itasimama kidete kukabiliana na njama zisizo na tija za mabeberu wa dunia.
Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran pia amesisitiza kuwa, mapatano ya JCPOA si mapatano ambayo yanahitajia saini au kuthibitishwa na mtu yoyote tu bali ni mapatano yaliyopasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na ni wajibu kuheshimiwa na kila mtu.
Vile vile amesema, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA umeshathibitisha mara 11 kuwa Iran imeheshimu kikamilifu mapatano ya nyuklia. Amesema: Natangaza kwa mara ya mwisho kwamba Iran haiwezi kamwe kudhoofisha usalama wake na wala haiko tayari kufanya mazungumzo kuhusu mapatano ambayo yamefikiwa kwa nia njama.