Velayati: Iran itachukua hatua inayofaa endapo Marekani itajiondoa katika makubaliano ya JCPOA
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa amesema kuwa, endapo Marekani itajiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatoa jibu mwafaka kulingana na mazingira yalivyo.
Dakta Ali Akbar Velayati amesema hayo jana alipotembelea maonyesho ya kimataifa ya vitabu mjini Tehran na kuwaambia waandishi wa habari kwamba, Iran iko tayari kuchukua uamuzi wowote ule kukabiliana na hatua ya Marekani ya kujitoa katika makubaliano ya nyuklia na Wamarekani wanaweza kujaribu waone.
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa amebainisha kwamba, kama Wamarekani watataka kujitoa katika makubaliano ya nyuklia au kuleta mchezo mwingine wa kisiasa na kutaka kuinyima Iran haki yake, bila shaka Jamhuri ya Kiislamu itachukua hatua mwafaka kwa mujibu wa mazingira yanayotawala na kuifanya Marekani ijute.
Ali Akbar Velayati amesema pia kuwa, kadhia kuu katika Mashariki ya Kati ni suala la Palestina na ameongeza kwamba, inasikitisha kuwa mwanzoni mwa karne ya ishirini baadhi ya wasaliti katika Mashariki ya Kati walishirikiana na Waingereza katika mpango wa kukaliwa kwa mabavu Palestina na Wazayuni.
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa ameeleza bayana kwamba, hii leo baadhi ya tawala zenye fikra mgando katika Mashariki ya Kati na hasa Saudi Arabia inashirikiana na Marekani kwa ajili ya kuhamishiwa huko Beitul-Muqaddas ubalozi wa Washington.