Ayatullah Khatami: Marekani na Umoja wa Ulaya hakuna wa kuaminiwa kati yao
Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran ameashiria kujiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na kusema kuwa, hakuna yeyote wa kuaminiwa, si Marekani wala Umoja wa Ulaya na kwamba, madola ya Ulaya hayana tofauti na serikali ya Washington katika kuhalifu ahadi.
Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amesema hayo leo mbele ya hadhara kubwa ya waumini waliohudhuria ibada ya kisiasa na kimaanawi ya Sala ya Ijumaa mjini Tehran na kusisitiza kwamba, uwezo wa makombora wa Iran hauihusu Marekani wala Umoja wa Ulaya.
Ayatullah Khatami amebainisha kwamba, endapo katika muda wa wiki kadhaa ambao Iran imeupatia Umoja wa Ulaya hasara ilizopata hazitafidiwa, Jamhuri ya Kiislamu haitabakia katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Khatibu wa leo wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran sambamba na kubainisha kwamba, tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, maadui daima wamekuwa wakifanya njama za kuupindua mfumo wa Kiislamu unaotawala hapa nchini amesema kuwa, maadui wanataka kuweko Iran ambayo ni dhaifu.

Ayatullah Khatami amesema bayana kwamba, Rais Donald Trump wa Marekani na baadhi ya nchi dhalili na duni katika Mashariki ya Kati zinachukia mno kuona Iran ina nguvu na haikubali kuburuzwa.
Kadhalika Khatibu wa Sala ya Ijumaa amesema kuwa Iran itaendelea na uwezo wake wa kijeshi na kwamba, kama utawala wa Kizayuni wa Israel utaleta wendawazimu, basi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaisawazisha na udongo miji ya Tel-Aviv na Haifa.
Ayatullah Khatami amesema pia kuwa, waungaji mkono wa Marekani na Israel katika Mashariki ya Kati ukiwemo utawala wa Aal-Saud, Bahrain na Imarati zinapaswa kutambua kwamba, endapo katika eneo hilo kutatotea jambo lolote dhidi ya Iran basi zenyewe zitakuwa za kwanza kufa kabla ya Marekani.