JCPOA; Siasa za Iran na matarajio yake kwa nchi Ulaya
Baada ya Marekani kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, mashauriano mapana, ya kina na ya nyuga tofauti yanaendelea kufanyika kwa madhumuni ya kuyadumisha makubaliano hayo kwa sharti la kudhaminiwa kivitendo manufaa na maslahi ya Iran. Na wakati nchi za Ulaya, China na Russia zinatangaza uungaji mkono wao kwa JCPOA, Marekani imetangaza vikwazo vingine vipya dhidi ya Iran.
Kwa kuutumia muda wa muhula wa wiki kadhaa uliotolewa na Iran kwa nchi za Ulaya kueleza bayana na kwa uwazi kabisa misimamo yao kuhusu makubaliano ya nyuklia na JCPOA na kuziba pengo lililoachwa na Marekani kwa kujiondoa kwenye makubaliano hayo, mashauriano mapana na ya kina kati ya nchi za Ulaya zilizomo kwenye JCPOA sambamba na mazungumzo kati ya Iran na nchi nyinginezo ghairi ya hizo yamekuwa yakiendelea. Baada ya kujitoa Marekani, maafisa wa ngazi za juu wa Iran wamesisitiza kwa uwazi kabisa kwamba ikiwa nchi tatu za Ulaya zilizomo kwenye JCPOA hazitatoa hakikisho la kivitendo, na Iran ikashindwa kupata manufaa kamili inayostahiki katika makubaliano hayo, watachukua maamuzi mazito kuhusu makubaliano hayo ya nyuklia.
Kutokana na kushadidi hali ya kutoaminiana inayotawala katika mfumo wa kimataifa iliyosababishwa na dharau iliyoonyeshwa na Marekani kwa makubaliano ya kimataifa yaliyothibitishwa na Umoja wa Mataifa, kuna ulazima wa kubainishwa na kueleweka wazi sera za nchi za Ulaya kuhusiana na JCPOA; na kwa mtazamo wa Iran haitoshi wala haikubaliki kusisitiza kwa maneno matupu kwamba zingali zinayaunga mkono makubaliano hayo ya nyuklia. Kuhusiana na jambo hilo, siku ya Alkhamisi, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, ambapo kwa mara nyingine tena alizitaka nchi za Ulaya zitangaze katika muda wenye mpaka maalumu, msimamo wao rasmi juu ya namna gani manufaa na maslahi ya Iran yatadhaminiwa na kupatikana katika JCPOA baada ya Marekani kujitoa kwenye makubaliano hayo ya kimataifa.
Katika mazingira yaliyopo ya baada ya Marekani kujitoa kwenye JCPOA, kuna ualzima kwa nchi za Ulaya zilizomo kwenye makubaliano hayo, yaani Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kutoa hakikisho kwamba Iran itanufaika kivitendo na kwa uwazi kabisa na makubaliano hayo ya nyuklia. Ni kama alivyosisitiza Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwamba, pasi na kuwepo hakikisho la uhakika na la kivitendo litakalotolewa na nchi hizo tatu za Ulaya haitowezekana kuyaendeleza makubaliano ya JCPOA.
Msimamo huo wa wazi umechukuliwa kutokana na tajiriba ya namna Marekani ilivyoyakanyaga makubaliano ya JCPOA; kwani licha ya kubeba dhima ya kuyatekeleza makubaliano hayo ya kimataifa, iliziba njia zote za kuiwezesha Iran kunufaika nayo, na mwisho wa yote ikaamua kujitoa moja kwa moja. Mtazamo ambao Marekani ilikuwa nao kuhusiana na Iran wakati ilipokuwemo kwenye makubaliano ya JCPOA, ndio inaoendelea kuufanyia kazi hivi sasa pia baada ya kujitoa kwenye makubaliano hayo. Siku ya Alkhamisi iliyopita, katika hatua ya kwanza kuchukuliwa baada ya kujitoa kwenye JCPOA, Wizara ya Fedha ya Marekani ilitangaza kuwa mashirika matatu na shakhsia sita wa Kiirani wanajumuishwa kwenye orodha yake ya vikwazo kwa kisingizio cha kuwa na uhusiano na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Sepah (IRGC). Kuwawekea vikwazo shakhsia na mashirika hayo kumeonyesha jinsi Marekani inavyouandama uwezo wa makombora wa Iran unaotokana na wataalamu wa ndani wa taifa hili na mchango athirifu na wenye faida unaotolewa na Iran katika eneo hili la Mashariki ya Kati. Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa akitaka kuyaingiza masuala ya makombora na ushawishi wa Iran katika eneo kwenye mazungumzo na makubaliano ya JCPOA; na alipoona kuwa hilo halitekelezeki ndipo akaamua kujitoa.
Kwa kuzingatia kwamba nchi tatu za Ulaya zilizomo kwenye makubaliano ya JCPOA, nazo pia zinaimba wimbo wa Trump kuhusu mpango wa makombora na nafasi ya Iran katika eneo kwenye kauli na matamshi yao, suala hilo limeufanya wasiwasi wa Tehran juu ya misimamo ya nchi hizo kuhusu makubaliano hayo ya nyuklia uwe mkubwa maradufu.
Katika kipindi hiki cha JCPOA bila ya kuwemo Marekani, matarajio yaliyopo ni kuziona Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zikichukua misimamo ya wazi; na katika matendo kuyatekeleza makubaliano hayo ya nyuklia pasi na kuyaingiza na kuyazungumzia mambo ya kando na yasiyohusika na JCPOA. Kuhusiana na hilo, serikali ya Iran imesisitiza kupitia taarifa yake kwamba: "Pande nyingine husika katika JCPOA na hasa nchi tatu za Ulaya zina wajibu wa kuchukua hatua zinazotakiwa kwa ajili ya kulinda JCPOA na kutekeleza majukumu yao bila ya masharti yoyote kuanzia awamu ya utoaji ahadi hadi awamu ya utekelezaji."
Makubaliano ya JCPOA yanayotakiwa na Iran, ni yale ambayo licha ya kujitoa Marekani, yatadhamini kikamilifu manufaa na maslahi ya kiuchumi ya Iran (kuanzia ya uuzaji wa mafuta yake mpaka kwenye uhusiano wa kibenki na kushiriki makampuni na mashirika ya kimataifa katika uwekezaji hapa nchini). Na wala makubaliano hayo yasibaki kuwa jina tupu kwa visingizio hivi na vile vikiwemo vya ushawishi wa kieneo wa Iran na mpango wake wa makombora; bali muhimu zaidi ni kutotumia kisingizio cha kurejeshwa vikwazo vya upande mmoja vya Marekani. Katika hali kama hii ikiwa baada ya kufanya mashauriano ya wiki kadhaa na nchi tatu za Ulaya, serikali ya Iran itafikia hitimisho kwamba JCPOA haidhamini manufaa na maslahi ya taifa hili hakuna shaka yoyote kuwa itaangalia tena sera zake na kuchukua uamuzi mpya.../