Zarif: Russia yasema itaheshimu mapatano ya nyuklia hata baada ya Marekani kujiondoa
(last modified Mon, 14 May 2018 13:35:18 GMT )
May 14, 2018 13:35 UTC
  • Zarif: Russia yasema itaheshimu mapatano ya nyuklia hata baada ya Marekani kujiondoa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif amesema Russia imethibitisha kuwa itaendelea kuheshimu mapatano ya nyuklia ya Iran ambayo ni maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, JCPOA, hata baada ya Marekani kujiondoa.

Zarif ameyasema hayo leo mjini Moscow baada ya mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov ikiwa ni duru ya pili ya safari yake kuhusu mapatano hayo ya nyuklia. Zarif amesema Russia na Iran zimeafiki kuhakikisha mapatano hayo yanalindwa wiki moja tu baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza kuwa nchi yake inajiondoa katika mapatano hayo ya kimataifa yaliyofikiwa baina ya Iran na nchi sita kubwa duniani ambazo ni wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Ujerumani.

Zarif ambaye kabla ya kufika Moscow alikuwa nchini China amesema lengo la mazungumzo yake ni kupata dhamana kuwa maslahi ya taifa la Iran yatalindwa. Kwa upande wake, Lavrov amesema nchi yake itashirikiana na Umoja wa Ulaya  kwa lengo la kulinda maslahi ya mapatano ya Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif na mwenzake wa China Wang Yi

Lavoro ameongeza kuwa ni jambo la kusiktisha kuwa Marekani inakiuka mapatano ya kimataifa kama hayo ya JCPOA na pia imekiuka maafikiano ya kimataifa kuhusu kadhia ya Quds (Jerusalem) na mikataba mingine mingi ya kimataifa. Ameelezea matumaini yake kuwa kutatumiwa mbinu za kulinda mapatano ya nyuklia ya Iran kwa kushirikisha nchi tatu za Ulaya ambazo ni Ujerumani, Uingereza na Ufaransa na pia kwa kujumuisha pande zingine katika mapatano hayo ambazo ni Russia, China, Iran na Umoja wa Ulaya. Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia pia amesema Iran ina haki ya kutetea haki zake za kisheria kwa mujibu wa mapatano hayo ya nyuklia. Baada ya Moscow, Zarif ataelekea Brussels kwa lengo la kufanya mazingumzo na Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya Federica Mogherini na pia mawaziri wa mambo ya nje wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.

Tags