Spika wa Bunge la Iran awatumia salamu za Ramadhani maspika wa mabunge
(last modified Wed, 16 May 2018 14:08:30 GMT )
May 16, 2018 14:08 UTC
  • Spika wa Bunge la Iran awatumia salamu za Ramadhani maspika wa mabunge

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, Ali Larijani amewatumia maspika wa mabunge ya nchi za Kiislamu salamu kwa mnasaba wa kuwadia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Katika aghalabu ya nchi za Kiislamu, ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Alkhamisi Tarehe 17 Mei 2018 itakuwa ni siku ya kwanza ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Katika ujumbe wake huo leo Jumatano, Larijani amesema: "Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni fursa nzuri ya kuimarisha mshikamano na umoja miongoni mwa mataifa ya Waislamu na kutatua hitilafu zilizopo katika jamii za Kiislamu."

Spika wa Bunge la Iran ameongeza kuwa: "Mshikamano na muungano wa nchi za Kiislamu ni mambo ambayo yataleta usalama na utulivu endelevi katika ulimwengu wa Kiislamu."

Spika wa Bunge la Iran Ali Larijani

Larijani amesisitiza kuwa: "Bunge la Iran linaunga mkono kuimarishwa ushirikiano zaidi miongoni mwa mabunge ya nchi za Kiislamu kwa lengo la kuleta umoja na mshikamano ili hatimaye kuondoa hitilafu na vitisho vilivyopo katika umma wa Kiislamu."

Spika wa Bunge la Iran amewatakia Waislamu wote duniani kheri na  fanaka katika Mwezi Mtukufuw a Ramadhani.

Tags