Russia: Vikwazo vya Marekani haviwezi kuizuia Moscow kushirikiana na Iran
Naibu Waziri Mkuu wa Russia amesema kuwa, vikwazo vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haviwezi kuzuia ushirikiano kati ya Moscow na Tehran.
Dmitry Kozak, ameyasema hayo akizungumza na Shirika la Habari la TASS la Russia kwa kusema: "Sisi tungali tunafuatilia suala hilo na tunafanya juhudi kubwa angalau kwa uchache tuweze kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na vikwazo hivyo katika mahusiano yetu na Iran."
Kozak amebainisha kwamba serikali ya Russia inatambua kuwa ni hatari kuendesha shughuli za kibiashara nchini Iran kwa kutumia mabadilishano ya sarafu ya dola na ameongeza kwamba, sekta ya biashara ya Russia ina uwezo wa kwenda sambamba na mazingira mapya sanjari na kubuni njia za utatuzi kwa ajili ya kuendeleza ushirikiano huo wa kibiashara na Tehran. Naibu Waziri Mkuu wa Russia pia ameashiria utilianaji saini wa makubaliano ya kuanzisha eneo maalumu la uhuru wa kibiashara kati ya Iran na Umoja wa Kibiashara wa Eurasia, uliofikiwa nchini Kazakhstan na kusema, makubaliano hayo ni harakati nzuri katika mabadilishano ya kibiashara na shughuli za kimasoko za nchi wanachama.
Inafaa kukumbusha kwamba Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuiondoa nchi yake katika makubaliano ya nyuklia ya Iran JCPOA, tarehe nane mwezi huu sambamba na kutoa tuhuma bandia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sambamba na hatua hiyo alitoa amri ya kurejeshwa vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran katika kipindi cha kati ya miezi mitatu hadi sita, hatua ambayo imeendelea kukosolewa katika nyuga mbalimbali za kimataifa kutokana na uvunjaji wa wazi wa mikataba uliofanywa na Marekani.