Iran haitafanya mazungumzo kuhusu maudhui yoyote isipokuwa Mapatano ya Nyuklia ya JCPOA
Karibu wiki mbili baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekeelzwaji, JCPOA, kumefanyika mazungumzo mjini Brussels baina ya wakuu wa Iran na Umoja wa Ulaya.
Umoja wa Ulaya umetoa taarifa baada ya kikao hicho cha Brussels na kutangaza kuunga mkono wake kikamilifu kwa mapatano ya JCPOA. Pamoja na hayo, hadi pale kutakapopatikana uhakika kamili kuhusu kulindwa maslahi ya Iran katika JCPOA, hakuna hakikisho lolote kuhusu kubakia Iran katika mapatano hayo.
Kwa msingi huo na katika fremu iliyoainishwa katika mazungumzo ya Iran na nchi za Ulaya, ni masuala yanayohusiana na JCPOA tu ndiyo yatakayojadiliwa katika mazungumzo baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na pande nyingine zilizobakia katika mapatano hayo baada ya Marekani kujiondoa. Mkutano huo wa kitaalamu wa Kamati ya Pamoja ya JCPOA utafanyika Ijumaa Mei 26 na utakuwa wa kwanza kufanyika pasina Marekani kuwepo katika kikao hicho. Pande nyingine zilizosalia katika JCPOA mbali na Iran ni pamoja na China, Russia, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani pamoja na Umoja wa Ulaya.
Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran jana Jumapili alijibu baadhi ya habari za vyombo vya habari vya kigeni kuhusu kupewa Iran kifurushi kipya cha mkabala wa mapatano mapya ya nyuklia na kusema: "Habari na madai kama hayo yasiyo na msingi yamezushwa na duru za kipropangada za vyombo vya habari vya Kizayuni na wazushi wengine wa kimataifa ambao hawalitakii mema taifa la Iran kwa lengo la kuzusha mazingira hasi na kupotosha mkondo wa mazungumzo ya Iran na pande nyingine katika JCPOA."
Msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tokea yaanze kutekelezwa mapatano ya JCPOA umekuwa wazi. Iran kama moja ya pande zilizoafiki JCPOA imetekeleza ahadi zote na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA umewasilisha ripoti 11 kuthibitisha hilo. Pamoja na hayo, baada ya Marekani kuchukua uamuzi wa upande moja na ulio kinyume cha sheria wa kujiondoa katika mapatano hayo ya kimataifa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa itakablia katika mapatano ya JCPOA maadamu maslahi yake yatalindwa.
Mohammad Taher Kanani, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema hivi kuhusu mambo ambayo Marekani imetabiri nchi za Ulaya zitayatekeleza katika kuyalinda mapatano ya JCPOA. "Iwapo Trump atayawekea vikwazo mashirika ya Ulaya na China na azuie kuwepo mahusiano ya kibiashara kati ya Iran na Ulaya, huo utakuwa ni ukiukwaji mkubwa wa hati ya Shirika la Biashara Duniani WTO na msingi wa biashara huru na hivyo nchi za Ulaya zinaweza kuishtaki Marekani katika WTO."
Hadi sasa nchi za Ulaya hazijachukua msimamo wa wazi na zinachukua misimamo inayogongana. Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akizungumza Jumapili katika mkutano wake na Miguel Arias Canete, Kamishna wa Nishati katika Umoja wa Ulaya alisema: "Tangazo la EU la kuheshimu mapatano ya nyuklia ya Iran yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA) sambamba na hatua tarajiwa ya mashirika makubwa ya Ulaya kusitisha ushirikiano na Iran ni mambo yanayokinzana."

Naye Kamal Kharrazi, Mkuu wa Baraza la Kiistratijia la Sera za Kigeni la Iran katika mazungumzo yake na gazeti la Kiitaliano la Corriere della Sera amesema hivi kuhusu hatima ya JCPOA: "Kulindwa mapatano ya nyuklia ya Iran kutategemea muelekeo wa nchi za Ulaya na iwapo bara Ulaya halitajihami mbele ya vitisho, basi mustakabli utakuwa mgumu."
Kuwepo misimamo inayokinzana ya Umoja wa Ulaya kuhusu maamuzi ya upande moja ya Marekani dhidi ya Iran ni jambo linalotilia shaka iwapo stratijia za umoja huo zimeweza kuwa na faida. Nchi za Ulaya zinapaswa kutoa dhamana imara zaidi kuwa zinaweza kulinda maslahi yao na yale ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hadi mwisho.