Rouhani: Dunia imetambua rasmi haki za nyuklia za Iran
Rais Hassan Rouhani wa jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa walimwengu na jumuiya za kimataifa zimetambua rasmi haki za Iran katika uwanja wa nyuklia.
Rais Rouhani ambaye mapema leo amehutubia maonyesho ya mafanikio ya nyuklia ya Iran amesema kuwa, dunia imekiri kwamba miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran inafanyika kwa malengo ya amani na ndiyo maana imeanza kushirikiana na Tehran katika uwanja huo.
Amesema walimwengu wameona kwamba nguvu ya mantiki katika meza ya mazungumzo imeshinda vitisho na mashinikizo na hapana shaka kwamba, mafanikio ya wanadiplomasia wa Iran katika mwaka uliopita katika meza ya mazungumzo ya nyuklia na nchi za kundi la 5+1 ni miongoni mwa matunda muhimu zaidi ya kidiplomasia ya Iran katika karne hii.
Rais Rouhani ametilia mkazo udharura wa kuamiliana na dunia na wakati huo huo kufanya jitihada kubwa za kujitosheleza na kusema kuwa, juhudi za kufikia kiwango cha kujitosheleza zinapaswa kufanyika kwa gharama ya chini na muda mfupi. Amesisitiza kuwa Iran ni nchi inayotetea haki zake na pale inapolazimu itatumia zana nyepesi na ngumu katika kutetea na kulinda haki zake.
Matamshi hayo ya Rais Hassan yametolewa kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia.
Kesho tarehe 20 Farfardin mwaka wa Hijria Shamsia sawa na Aprili 9 huadhimishwa hapa nchini kama Siku ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia.