Qassemi: Magaidi wamedhamiria kuvuruga uthabiti na usalama wa Afghanistan
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani shambulio la kigaidi lililotokea jana katika jimbo la Nangarhar nchini Afghanistan na kutuma salamu za kuifariji serikali na wananchi wa nchi hiyo.
Huku akisisitiza kwamba magaidi wamedhamiria kuvuruga uthabiti na usalama wa Afghanistan, Bahram Qassemi amesema, wasiolitakia mema taifa la Afghanistan, ambao wanahisi uthabiti, utulivu na juhudi zilizofanywa hivi karibuni zikiwemo za kusitishwa vita kati ya serikali na kundi la Taliban vinakinzana na maslahi yao, hawawezi kuvumilia kuona umoja unapatikana nchini humo; kwa hivyo wamefanya jinai nyingine ili kuonyesha kwamba kuendelea kuwepo kwao kunategemea utendaji jinai na kuzusha mifarakano nchini.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, baada ya muda si mrefu serikali na wananchi wa Afghanistan wataweza kuwashinda magaidi hao wanaovuruga umoja, uthabiti na usalama na kuonja matunda ya subira na muqawama wao kwa ushindi watakaopata dhidi ya ugaidi.
Watu 22 waliuawa na wengine 34 walijeruhiwa jana jioni katika mripuko wa bomu uliotokea mahali kilipokuwa kikifanyika kikao cha wajumbe wa kundi la Taliban na wa vikosi vya usalama vya serikali ya Afghanistan katika jimbo la Nangarhar mashariki mwa nchi hiyo.
Kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS) limetangaza kuwa ndilo lililofanya jinai hiyo.
Mripuko huo ulitokea wakati idadi kadhaa ya raia, askari wa serikali na wanachama wa Taliban walipokuwa wamejumuika pamoja kwenye mji wa Ghazi Amanullah katika jimbo la Nangarhar kusherehekea Sikukuu ya Idul-Fitri baada ya kutangazwa usitishaji mapigano kati ya serikali na kundi la Taliban kwa heshima ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na sikukuu tukufu ya Idul-Fitri.../