Iran yataka mapatano ya kusimamisha mapigano yaendelee nchini Afghanistan
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, Tehran imefurahishwa sana na mapatano ya kusimamisha mapigano baina ya kundi la Taleban na serikali ya Afghanistan kwa mnasaba wa sikukuu ya Idul Fitr na ina hamu ya kuona mapatano hayo yanaendelea.
Bahram Qassemi amesema hayo leo na kuongeza kuwa, kuendelea makubaliano hayo ya kusimamisha vita kunaweza kuwa mwanzo wa mchakato mpya na muhimu wa mazungumzo ya amani na hatimae kupatikana utulivu na amani ya kudumu huko Afghanistan.
Tarehe 12 mwezi huu wa Juni, serikali ya Afghanistan ilifikia mapatano ya kusimamisha vita na kundi la Taleban kwa muda wa wiki moja kwa mnasaba wa maadhimisho ya sikukuu ya Idul Fitr.
Hivi sasa serikali ya Afghanistan imetangaza kwa upande wake kuwa inapenda kuonda mapatano ya kusimamisha vita kati yake na kundi la Taleban yanaendelea kwa muda usiojulikana inagawa hata hivyo kundi la Taleban limesema, halina nia ya kuendelea na mapatano hayo kwa zaidi ya siku tatu.
Rais Muhammad Ashraf Ghani wa Afghanistan jana usiku alitoa ujumbe maalumu na kuviamrisha vikosi vya ulinzi na usalama vya nchi hiyo kuendeleza usimamishaji vita na kundi la Taleban hadi siku ya Jumatano wiki hii.