IRGC: Iran ipo tayari kukabiliana na ugaidi wa kibiolojia
Kamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) ameashiria hatua zilizochukuliwa na Sepah kwa ajili ya kuzima jaribio lolote la shambulizi la kibiolojia na kusema kwamba, kitengo cha usalama cha jeshi hilo kimekuwa kikitoa mafunzo sambamba na kuzalisha zana za kukabiliana na ugaidi wa kibiolojia.
Jenerali Ali Nasiri amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Tasnim na kuongeza kuwa, mashambulizi ya kibiolojia ni mashambulizi mapya na yenye sura tofauti, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejiandaa vilivyo kukabili vitisho vyovyote dhidi yake.
Jenerali Nasiri ambaye ni Mkuu wa Idara ya Usalama ya IRGC amesema vyombo vya usalama hapa nchini vimejiweka tayari kuzima hujuma yoyote ya kibiolojia, haswa dhidi ya viongozi na wanasayansi wake.
Amesema kitengo cha kupambana na ugaidi hatari wa kibiolojia hapa nchini kimepokea suhula zote zinazohitajika huku watalaamu katika uga huo pia wakipokea mafunzo ya kiwango cha juu.
Itakumbukwa kuwa, Julai mwaka 2016, Brigedia Jenerali Gholam Reza Jalali, Mkuu wa Shirika la Ulinzi wa Raia wa Iran alitoa mwito wa kuchukuliwa hatua zote hitajika kwa ajili ya kuwalinda wananchi wa Iran kutokana na shambulizi lolote la kemikali, mbinu mpya inayotumiwa na magenge mbalimbali ya kigaidi duniani.