Brigadia Jenerali Salami: Adui anaogopa kuingia vitani na Iran
Naibu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran amesema kuwa, adui amepoteza uwezo wake wote wa kuingia vitani na Iran na kwamba amechakaa na karibu atatokomea.
Brigedia Jenerali Hussein Salami amesema sababu ya adui kujiepusha kuingia vitani na Iran ni uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kuwa, adui anajua vyema kwamba, kuanzisha vita dhidi ya Iran kuna taathira mbaya za kimataifa na kutabadili mlingano wa nguvu kote duniani.
Naibu Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, ushawishi wa Iran katika eneo la Mashariki ya Kati ni wa kiroho na hauwezi kufutwa, na adui anafanya kila awezalo kutoa pigo kwa Jamhuri ya Kiislamu kupitia njia ya kupunguza ushawishi wake wa kikanda.
Brigedia Jenerali Salami amesema Marekani imetumia dola bilioni elfu saba huko Iraq na Syria na haikupa faida yoyote kama alivyokiri Rais Donald Trump wa nchi hiyo, na suala hilo ni ishara kwamba, Iran imepata ushindi katika eneo hili.
Amesisitiza kuwa muqawama na mapambano ya Kiislamu yamekaribia zaidi kwenye mipaka ya utawala wa Kizayuni wa Israel, na Marekani na Magharibi kwa ujumla wameshindwa kukabiliana na wimbi hilo lenye nguvu la kimataifa.