Iran yazima njama ya magaidi wakufurishaji kujipenyeza nchini
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i46340-iran_yazima_njama_ya_magaidi_wakufurishaji_kujipenyeza_nchini
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limetangaza kufanikiwa kuwazuia magaidi wakufurishaji kujipenyeza katika eneo la Mirjaveh kusini mashariki mwa nchi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 26, 2018 07:50 UTC
  • Iran yazima njama ya magaidi wakufurishaji kujipenyeza nchini

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limetangaza kufanikiwa kuwazuia magaidi wakufurishaji kujipenyeza katika eneo la Mirjaveh kusini mashariki mwa nchi.

Katika taarifa, Idara ya Mahusiano ya Umma ya Kituo cha Quds cha Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu imetangaza kuwa, "Jumatatu usiku, kundi moja la magaidi wakufurishaji lilikusudia kutumia eneo la Mirjaveh mkoani Sistan na Baluchistan kujipenyeza katika ardhi ya Iran kwa lengo la kutekeleza hujuma za kigaidi lakini kutokana na kuwa macho askari wa eneo hilo la mpakani, magaidi hao walizuiwa na idadi kadhaa miongoni mwao kuuawa."

Duru zinadokeza kuwa magaidi wasiopungua watatu waliangamizwa  katika ufyatulianaji risasi na wanajeshi wa Iran huku  wengine wakijeruhiwa na baadhi wakitoroka na kurejea Pakistan walikotokea.

Aidha katika oparesheni hiyo wakaazi wawili wa eneo hilo ambalo walikuwa katika kikosi cha kujitolea cha wananchi, Basiji, na askari mmoja wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu waliuawa shahidi katika mapigano hayo.

Kituo cha Quds cha Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kimetangaza kuwa walinzi wa mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wawe ni wanajeshi, polisi au wananchi walio katika kikosi cha kujitolea cha wananchi, Basiji, wako tayari kukabiliana na aina zote za chokochoko za maadui wa mapinduzi na taifa la Iran. Amesema ardhi ya Iran itakuwa sehemu ya kuwaangamiza magaidi na mamluki wa madola ya kiistikbari.