Larijani: Taifa la Iran halikubali kupiga mnada heshima yake
Ali Larijani Spika wa Bunge la Iran, Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, amesema Wairani ni taifa lenye subira na lenye kupenda kuwa na uhusiano na wengine lakini hawapigi mnada heshima yao.
Larijani ameyasema hayo leo asubuhi katika kikao cha bunge na kuongeza kuwa: "Hata kama adui anafuatilia nadharia ya mashinikizo na mbano wa kiuchumi dhidi ya Iran, lakini taifa la Iran na sekta zote za serikali zimebadilisha njama hizo kuwa duru ya ujenzi mpya wa uchumi."
Spika wa Bunge ameongeza kuwa, leo Iran ina uwezo mkubwa wa kujihami na hivyo maadui sasa hawatafakari kuhusu vita dhidi ya Iran bali wanazungumzia kupunguza uwezo wa makombora ya Iran. Amesema uwezo huo wa makombora umetokana na jitihada za ndani ya nchi.
Spika wa Bunge la Iran ameashiria masuala ya kieneo na kusema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miaka ya hivi karibuni imejitahidi kukandamiza harakati haribifu za magaidi ili magaidi hasa wa ISIS au Daesh wasiweze kuvuruga usalama wa eneo. Amesema wote wanafahamu kuwa magaidi katika eneo wamekuwa wakiungwa mkono na madola makubwa pamoja na baadhi ya tawala zisizo na busara katika eneo lakini kutokana na kusimama kidete mataifa, magaidi wameshindwa.
Larijani aidha ameashiria kupitishwa sheria ya kibaguzi ya 'Nchi ya Mayahudi', katika bunge la utawala haramu wa Israel, Knesset, na kusema: "Uamuzi huo wenye chuki wa bunge la utawala wa Kizayuni ni ishara kuwa Marekani na utawala wa Kizayuni zinafanya kila ziwezalo kuvuruga usalama wa eneo."