Abdolreza Rahmani Fazli: Marekani haiwezi kuthubutu kukabiliana kijeshi na Iran
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran amesema kuwa, Marekani haiwezi kuthubutu katu kukabiliana kijeshi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Abdolreza Rahmani Fazli amesema hayo katika mji wa Orumiyeh kaskazini magharibi mwa Iran na kueleza kuwa, Wamarekani wanaelewa vyema kwamba, endapo wataanzisha vita basi mmalizaji wa vita hivyo haiwezi kuwa Marekani.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran amesema bayana kwamba, viongozi wa Marekani wamesimama kwa ajili ya kukabiliana kijeshi, kijamii na kiuchumi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini wanajua vyema kwamba, hawawezi kufanya chochote katika uga wa kijeshi.
Kuhusiana na suala la mazungumzo kati ya Marekani na Iran, Abdolreza Rahmani Fazli ameashiria suala la kutoaminika Marekani sambamba na kukiuka ahadi na mapatano viongozi warongo wa Washington na kusema kuwa, kurejea Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuwaomba msamaha walimwengu ndio masharti muhimu ya Tehran kwa ajili ya kufanya mazungumzo na taifa hilo.
Rahmani Fazli amesema kuwa, kuzusha mizozo ya kijamii ni miongoni mwa mambo yanayozingatiwa na Marekani kwa ajili ya kukabiliana na taifa la Iran na kueleza kuwa, Wamarekani wanajidanganya kwa kudhani kwamba, wanaweza kuvuruga hali ya mambo nchini Iran na wanapoteza muda wao bure kwa kufanya vikao na maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwani njama zote hizo zitashindwa.