Iran yalaani hujuma ya kigaidi dhidi ya msikiti nchini Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i47218-iran_yalaani_hujuma_ya_kigaidi_dhidi_ya_msikiti_nchini_afghanistan
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani hujuma ya kigaidi dhidi ya msikiti mmoja wakati wa Swala ya Ijumaa katika mkoa wa Paktia mashariki mwa Afghanistan.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Aug 04, 2018 03:34 UTC
  • Iran yalaani hujuma ya kigaidi dhidi ya msikiti nchini Afghanistan

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani hujuma ya kigaidi dhidi ya msikiti mmoja wakati wa Swala ya Ijumaa katika mkoa wa Paktia mashariki mwa Afghanistan.

Katika taarifa, Bahram Qassemi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametangaza mfungamano wa Iran na watu na serikali ya Afghanistan hasa familia za waathirika wa hujuma hiyo ya kigaidi na kusema: "Ugaidi ulioingiziwa kutoka nje na kulazimishwa kwa watu wa Afghanistan unalenga kuibua mifarakano kwa kuvuruga usalama katika taifa hilo. Hivyo ametoa wito kwa serikali ya Afghanistan  kuwa angalifu na itumie busara katika kuvunja njama hii na waliotenda jinai hiyo isiyo na mipaka wawajibishwe.

Siku ya Ijumaa ya jana magaidi waliingia ndani ya  Msikiti wa Imam Zaman (ATF) katika eneo la Khawaja Hassan mjini Gardez, ambapo walifyatua risasi na kujilipua miongoni mwa waumini waliokuwa wakiswali Swala ya Ijumaa.

Taarifa zinasema waumini 31 waliokuwa wakiswali waliuawa na wengine 81 kujeruhiwa. Baada ya hujuma hiyo, kundi la Taliban lilitoa taarifa na kusema halijahusika. Kundi la kigaidi la ISIS au Daesh ndilo ambalo kawaida hutangaza kuhusika na hujuma dhidi ya misikiti nchini Afghanistan.

Magaidi wa ISIS wanaopata himaya ya Marekani nchini Afghanistan

Zamir Kabulov, mjumbe maalumu wa rais wa Russia katika masuala ya Afghanistan hivi karibuni alitangaza kuwa kuna ushahidi unaoonyesha kwamba Marekani ikishirikiana na muungano wa kijeshi wa NATO inahusika katika kuwaingiza magaidi wa ISIS nchini Afghanistan kutoka Syria na Iraq.

Viongozi na wananchi wa Afghansitan pia wamebainisha wazi kuwa Marekani inaunga mkono kuenea kundi la ISIS nchini humo. 

Marekani na waitifaki wake walivamia Afghansitan mwaka 2001 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kurejesha usalama lakini hivi sasa si tu kuwa ugaidi umeongezeka katika nchi hiyo bali pia kumeshuhudiwa pia ongezeko kubwa la ukulima na uzalishaji wa dawa za kulevya.