Trump aendelea kutoa vitisho dhidi ya washirika wa kibiashara wa Iran
Rais Donald Trump wa Marekani amezitishia tena nchi zenye uhusiano wa kibiashara na Iran baada ya kupuuzwa amri aliyotoa ya kutekelezwa tena vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Trump ameandika kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Twitter kuwa: nchi yoyote itakayofanya biashara na Iran haitofanya biashara na Marekani.
Trump ameashiria kuanza rasmi tena kutekelezwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran na kusema kuwa hivyo ni vikwazo vikali zaidi kuwahi kuwekwa hadi sasa.
Rais wa Marekani ameendelea kusema kuwa duru nyingine ya vikwazo dhidi ya Iran itatekelezwa mnamo mwezi Novemba.
Umoja wa Ulaya na nchi tatu za umoja huo ambazo ni wadau katika makubaliano ya nyuklia ya Iran ya JCPOA, yaani Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimepuuza vitisho hivyo vya Trump na kutangaza kuwa sambamba na kuanza kutekelezwa vikwazo hivyo vya Marekani, nazo pia zimetekeleza kanuni za uzuiaji vikwazo, za kukabiliana na vikwazo hivyo na kuzihami shughuli za kibiashara za mashirika ya Ulaya yaliyoko nchini Iran.
Serikali ya China nayo pia imetangaza kuwa haitaunga mkono vikwazo vya mafuta vya Marekani, bali itaendelea kununua mafuta kutoka Iran.../