Zarif: Kesi ya Iran dhidi ya Marekani ICJ ina nguvu sana
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema, kesi ya Iran dhidi ya Marekani katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu, ICJ, ina nguvu sana. Ameongeza kuwa Marekani sasa imejikita zaidi katika masuala ya kipropagnada kuhusu kesi hiyo.
Zarif ameashiria mashtaka yaliyowasilishwa na Iran katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu kutokana na hatua ya Washington ya kuiwekea nchi hii vikwazo vilivyo kinyume cha sheria na kusema: "Baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, na kurejesha tena vikwazo, Iran imewasilisha kesi ICJ kutokana na kuwa Marekani imekiuka mkataba wake na Iran uliotiwa saini mwaka 1955 kuhusu uhusiano mwema na uhusiano wa kiuchumi."
Zarif amesema, hata kama Marekani imezungumzia mazungumzo mapya baada ya kujiondoa katika JCPOA lakini ukweli unabakia kuwa imekiuka mapatano, na Iran imechukua hatua ya kufungua kesi hiyo kwa mujibu wa mkataba wa 1955.
Rais Donald Trump wa Marekani tarehe Nane Mei mwaka huu alikariri tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran na kutangaza kujitoa Washington katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA sambamba na kurejesha vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran. Hatua hiyo ya Trump ilikosolewa vikali ndani ya Marekani na katika uga wa kimataifa.
Mahakama ya ICJ imetangaza kupitia taarifa yake kuwa vikao vinne vitafanyika kwa siku nne mfululizo mjini The Hague yaani kuanzia Agosti 27 hadi 30 ili kusikiliza mashtaka yaliyowasilishwa na Iran dhidi ya Marekani.