Zarif: Viongozi wa Marekani wameelekeza zaidi fikra zao katika vita vya kisaikolojia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa viongozi wa Marekani wameelekeza zaidi fikra zao katika vita vya kisaikolojia huku wakifanya juhudi za kuzidisha mashinikizo ya kisaikolojia dhidi ya Wairani na washirika wa kimataifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Muhammad Javad Zarif amesema kuwa hali ya mambo hii leo imebadilika sana kwa kuzingatia Marekani kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na anga ya vita vya kisaikolojia iliyoibuliwa hivi sasa. Amesema hakuna makubaliano ya kimataifa ya pande kadhaa yanayozingatiwa na pande zote husika. Kama ambavyo Marekani inasema kuwa makubaliano ya JCPOA ni makubaliano mabaya zaidi katika historia na yameshindwa kudhamini maslahi yao yote.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa Iran inatofautiana na nchi nyingine katika eneo na kwamba nchi za eneo hili zinanunua silaha ili kudhamini usalama wa nchi zao huku Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiamini kuwa usalama, maendeleo na ustawi wake unafungamana na wananchi; na ndio maana katika kipindi chote cha miaka 40 Iran imekuwa ikikabiliwa na kila aina ya mashinikizo na wananchi wameweza kusimama imara na kukabiliana na mashinikizo hayo yote. Muhammad Javad Zarif amesisitiza kuwa Marekani imeshindwa kutimiza malengo yake tangu Rais wa nchi hiyo Donald Trump atangaze kujitoa katika makubaliano ya JCPOA na hivi sasa viongozi wa nchi hiyo wameamua kuchukua baadhi ya hatua zikiwemo za eti kutaka kufanya mazungumzo na kuunda kundi la uchukuaji hatua dhidi ya Iran.