Sergey Lavrov: Kuondoka mashirika ya Ulaya nchini Iran ni kosa kubwa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, sambamba na kuunga mkono ubunifu wa Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kuanzisha mfumo wa mabadilishano ya kifedha pamoja na Iran, amesema kuwa kuondoka mashirika ya Ulaya nchini Iran, ni kosa kubwa.
Sergey Lavrov ameyasema hayo akiongea na waandishi wa habari mjini New York, Marekani na kuongeza kuwa, Russia itashiriki katika kuanzishwa mfumo huo wa mabadilishano ya fedha kwa lengo la kuiepusha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi yake. Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameashiria kwamba kuiweka kando sarafu ya dola ya Marekani ni moja ya njia za kuiepusha Iran na vikwazo hivyo vya Marekani na kuongeza kuwa, kutumiwa sarafu za kitaifa katika miamala ya malipo kwa lengo la kupunguza kutegemea sarafu ya dola yaliyodumu kwa muda mrefu, ni jambo linalotekelezeka.
Sergey Lavrov ameongeza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeheshimu ahadi zake kuhusiana na mapatano ya nyuklia ya JCPOA na ni kwa ajili hiyo ndio maana Moscow inatumia uwezo wake wote kuyalinda makubaliano hayo ya kimataifa yaliyoidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Sambamba na kuunga mkono matamshi ya António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kuunga mkono azimio linalounga mkono haki ya kujitawala kila nchi ya dunia, amesema kuwa, iwapo kweli Marekani inaheshimu misingi ya kujitawala,basi haitakiwi kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine.