Kiongozi Muadhamu: Tunapaswa kuimarisha ulinzi usiohisika katika kukabiliana na vitisho vya maadui
(last modified Sun, 28 Oct 2018 16:15:13 GMT )
Oct 28, 2018 16:15 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Tunapaswa kuimarisha ulinzi usiohisika katika kukabiliana na vitisho vya maadui

Mkuu na maafisa wa Taasisi ya Ulinzi Usiohisika (Passive Defense) ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo wameonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

Katika mazungumzo hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia umuhimu mkubwa na unaozidi kuongezeka siku baada ya siku wa kuwa na ulinzi wa kimya kimya na usiohisika kwa ajili ya kuzuia mashambulizi ya maadui na kusisitiza kuwa: Ulinzi usiohisika inabidi ufanyike kwa ustadi mkubwa katika kukabiliana na mbinu tata za mashambulizi ya maadui na utekelezwe kivitendo na kwa umakini mkubwa na uende na wakati.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduizi ya Kiislamu katika mazungumzo ya karibu na maafisa wa Taasisi ya Ulinzi Usiohisika (Passive Defense) ya Iran

 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataka viongozi na maafisa wa sekta zote nchini Iran kuupa umuhimu unaotakiwa ulinzi wa aina hiyo na kusisitiza kuwa: Kama viongozi wa Iran watashindwa kujua umuhimu wa ulinzi huo na wakashindwa kuuimarisha kwa sura inayotakiwa, basi Iran itakuwa katika hatari ya kukumbwa na vitisho ambavyo baadhi yake itakuwa haviwezi kufidika. Hivyo amesema, viongozi na maafisa wa sekta mbalimbali nchini Iran iwe ni sekta za kijeshi au zisizo za kijeshi, wote wanapaswa kushirikiana kikamilifu katika kuimarisha ulinzi wa namna hiyo.