Oct 30, 2018 08:00 UTC
  • Zarif: Hakuna dhalimu yeyote awezaye kuyazima mapambano ya kupigania uadilifu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Hakuna dhalimu yeyote awezaye katu kuyazima mapambano ya kupigania uadilifu.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Twitter kwa mnasaba wa Arubaini ya Imam Hussein (as).

Katika ujumbe wake huo Zarif amesisitiza kuwa: Ujumbe wa watu milioni 17 wanaokutana Karbala kutoka duniani kote ni kwamba: Hakuna dhalimu yeyote awezaye katu kuyazima mapambano ya kupigania uadilifu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif

Ujumbe huo wa Dakta Zarif umeongezea kwamba: Karne 14 zilizopita, mtawala mmoja dhalimu aliamini ameweza kuuzima muqawama wa Imam Hussein. Saddam, Al-Qaeda na Daesh, nao pia walidhani wataweza kuumaliza muqawama huu.

Dakta Zarif amefafanua katika ujumbe wake huo kuwa: Pamoja na hayo, leo hii watu milioni 17 kutoka ulimwenguni kote  wakiwemo milioni mbili kutoka Iran wanakusanyika Karbala; na ujumbe wao ni kwamba: Hakuna dhalimu yeyote awezaye katu kuyazima mapambano ya kupigania uadilifu.

Wafanyaziara, wakiwemo walemavu, wanaotembea kwa miguu kuelekea Karbala

Leo Jumanne ni mwezi 20 Mfunguo Tano Safar inayosadifiana na maadhimisho ya Arubaini ya Imam Husain AS na wafuasi wake waaminifu ambayo imekuwa ikiadhimishwa tangu walipouawa shahidi watukufu hao miaka 1379 iliyopita. Mjukuu huyo wa Bwana Mtume Muhammad SAW aliuawa shahidi mwaka 61 Hijria katika jangwa la Karbala nchini Iraq.../

 

Tags