Dakta Zarif: Jamii ya Kimataifa imesimama dhidi ya vikwazo vya Marekani
-
Dakta Muhammad Javad Zarif
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, jamii ya kimataifa imesimama dhidi ya vikwazo vya Marekani kiasi kwamba, majirani na nchi za Ulaya zimesimama kidete dhidi ya hatua za upande mmoja za serikali ya Washington.
Dakta Muhammad Javad Zarif amesema hayo pambizoni mwa mkutano wa pande tatu mjini Istanbul wa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Azerbaijan na Uturuki na kuongeza kuwa, uamuzi wa Marekani wa kuiwekea vikwazo Iran ni kinyume na sheria na ada za kimataifa lakini inasikitisha kuwa, Washington ambao yenyewe inakiuka sheria ndiyo inayoziadhibu nchi nyingine ambazo kimsingi zinaheshimu na kutekeleza sheria.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuwa, licha ya Marekani kuiwekea vikwazo visivyo vya kisheria Tehran lakini imeshindwa kufikia malengo yake iliyokuwa imejiwekea.
Dakta Zarif amesema kuwa, Uturuki na Azerbaijan ni miongoni mwa nchi ambazo zinaunga mkono misimamo ya Iran kuhusiana na vikwazo vya Marekani na kusisitiza kwamba, nchi hizo zitaendeleza ushirikiano wao na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Dakta Muhammad Javad Zarif juzi Jumatatu alielekea nchini Uturuki akiuongoza ujumbe wa ngazi za juu wa Iran kwa ajili ya kwenda kushiriki katika kikao cha pande tatu cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Uturuki na Azerbaijan huko Istanbul.
Kwa mujibu wa Dakta Zarif miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa katika mkutano huo wa pande tatu ni ushirikiano wa pande husika katika uga wa elimu, utalii na nishati