Rais Rouhani: Iran haitasalimu amri mbele ya Marekani
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taifa hili litabakia kuwa huru na lenye mamlaka yake na katu halitasalimu amri mbele ya Marekani.
Rais Rouhani amesema hayo leo katika hadhara kubwa ya wananchi wa mkoa wa Azerbaijan Magharibi wa kaskazini magharibi mwa Iran ambapo sambamba na kubainisha kwamba, maadui kwa kutumia mashinikizo ya kiuchumi na kuwaletea matatizo wananchi hawataweza kuwafanya wananchi wa taifa hili wasisonge mbele katika malengo yao amesisitiza kuwa, wananchi wa Iran wataadhimisha mwaka wa 40 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa nguvu na ufanisi mkubwa na kulithibitisha hilo kivitendo kwa walimwengu wote.
Rais Hassan Rouhani amebainisha kuwa, nchi zote na mataifa yote ya dunia zinapinga hatua za kidhalimu za Marekani na kuongeza kuwa, Washington haiwezi kudhoofisha uhusiano wa Iran na mataifa mengine ndugu katika Mashariki ya Kati kwani Waislamu wote wako pamoja.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, kando na taifa la Iran kuna mataifa ya Iraq, Syria, Lebanon, Afghanistan, Pakistan na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla wanafikiria kusimama kidete, imani na mamlaka yao.
Aidha Rais Rouhani amebainisha kuwa, kusimama kidete mataifa ya Mashariki ya Kati kutapelekea kushindwa madola ya kibeberu duniani. Rais wa Iran kadhalika amesisitiza kuwa, maadui wamekasirishwa mno na juhudi za Iran za kuzuia magaidi kuwa na udhibiti katika Mashariki ya Kati na kueleza kwamba, Waislamu wakati wowote watakapotaka msaada wa Iran, basi Jamhuri ya Kiislamu itatekeleza jukumu lake kama inavyofanya katika vita dhidi ya ugaidi.