Ugaidi na kukaririwa njama zilizofeli za waungaji mkono ugaidi
Nchi za Magharibi na baadhi ya tawala za kiimla na vibaraka wao katika eneo la Mashariki ya Kati tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran zimekuwa zikiyaunga mkono na kuyasaidia makundi ya kigaidi kwa shabaha ya kutoa pigo kwa taifa la Iran.
Katika mkondo huo nchi za Magharibi na vibaraka wao ziliyaunga mkono na kuyasaidia kwa hali na mali makundi kama Munafiqeen (MKO), Daesh na lile linalojiita al Ahwaziyya na sasa magaidi waliofanya shambulizi la kigaidi huko Chabahar kusini mashariki mwa Iran. Ni vyema kukumbusha hapa kwamba, Alkhamisi ya jana gaidi mmoja aliyekuwa ndani ya gari lililokuwa na mabomu alikusudia kushambulia kituo cha polisi katika wilaya ya Chabahar mkoani Sistan na Baluchistan lakini alipokabiliwa na mapambano ya polisi wa eneo hilo alilipua gari lake mbele ya lango la kuingia kwenye kituo hicho. Watu wawili wameuawa shahidi katika shambulizi hilo na raia 40 wakiwemo wanawake na watoto wamejeruhiwa. Gaidi aliyefanya shambulizi hilo pia ameangamia.
Shambulizi hilo la kigaidi kwa mara nyingine tena limeonesha jinsi maadui walivyodhamiria kuvuruga usalama na amani nchini Iran. Ni wazi kuwa, maadui hao wa kieneo na kimataifa hawafurahishwi na usalama na maendeleo ya Jamhuri ya Kiislamu kwa sababu Iran ya Kiislamu inaendelea kusimama imara mbele ya mipango yao khabithi na inatoa kipigo baada ya kingine kwa makundi ya kigaidi wanayoyaunga mkono.
Si siri kwamba, kama alivyosema msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (Sepah), Ramadhan Sharif, makundi mengi ya kigaidi yana uhusiano na mashirika ya ujasusi ya nchi za kigeni kama Saudi Arabia na daima yamekuwa yakifanya njama za kutaka kuvuruga usalama katika maeneo ya mpakani ya Iran. Vilevile hakuna shaka kwamba, muungano wa kishetani wa pande tatu yaani Marekani, utawala wa kifalme wa Saudi Arabia na utawala haramu wa Israel una mfungamano mkubwa na matukio mengi ya kigaidi likiwemo la Alkhamisi ya jana katika eneo la Chabahar.
Ushahidi unaonesha kuwa, baadhi ya nchi za kidikteta za kusini mwa Ghuba ya Uajemi zinayafadhili na kuyasaidia makundi ya kigaidi huko kusini mashariki mwa Iran karibu na mpaka wa Pakistan. Itakumbukwa pia kwamba, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman aliwahi kusema bila ya kuona haya kwamba, atahamishia vita nchini Iran na daima amekuwa akiunga mkono harakati za kutaka kuundoa madarakani utawala wa Kiislamu hapa nchini.
Miongoni mwa malengo maovu ya hatua kama hizo ni kutaka kuyahusisha mashambulizi hayo ya kigaidi na masuala ya kikabila na kimadhehebu katika njama zinazopikwa na kubuniwa huko Washington, Riyadh na Tel Aviv. Mtaalamu wa masuala ya kimataifa, Sayyid Hadi Sayyid Afqahii anasema kuhusu njama za Marekani zinazofanyika kupitia mashambulizi kama haya kwamba: Matamshi ya Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu Iran yanapaswa kupewa mazingatio maalumu. Kiongozi huyo amesema mara kadhaa kwamba, atauondoa madarakani utawala wa Iran kwa njia yoyote ile inayowekana na mojawapo na njia hizo za Trump ni mashambulizi ya kigaidi kama hili la sasa. Trump ametishia mara kadhaa kwamba, Marekani inaweza kuzusha machafuko nchini Iran."
Malengo mengine ya shambulizi la jana huko Chabahar ni pamoja na kunyanyua juu moyo wa wanachama wa makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na mahasimu wa Jamhuri ya Kiislamu na kuvuruga uhusiano wa Iran na Pakistan.
Mji wa Chabahar ni miongoni mwa maeneo ya kichumi ya Iran ambako kumewekwa vitega uchumi vingi. Hivyo hapana shaka kuwa, wapangaji na watekelezaji wa shambulizi la kigaidi la jana wanataka kuvuruga usalama wa eneo hilo na kupunguza kasi ya ustawi wake wa kiuchumi.
Shambulizi hilo halina thamani yoyote katika upande wa masuala ya kijeshi na wala haliwezi kuwafikisha wapangaji wake kwenye malengo yao machafu. Pamoja na hayo tunapaswa kusisitiza kuwa, magaidi waliohusika na shambulizi hilo na waungaji mkono wao watalipa gharama kubwa. Ukweli huu umesisitizwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Muhammad Javad Zarif pale aliposema kwamba: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itawaburuta magaidi hao na mabwana zao kwenye uadilifu na jinai hiyo haitapita hivi hivi bila ya wahusika kuadhibiwa."