Qassemi: Uhusiano mzuri wa Iran na Iraq unaendelea
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, licha ya kuweko njama zisizo na natija za Marekani, uhusiano wa Tehran na Baghdad upo katika kiwango kizuri.
Bahram Qassemi amesema hayo leo katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari wa ndani na wa nje ambapo akijibu swali kuhusiana na kuongezeka mashinikizo ya Marekani dhidi ya serikali ya Iraq yenye lengo la kupunguza ushirikiano wake wa kiuchumi na Iran amesema kuwa, Iraq ni jrani mwema na mshirika wa kiuchumi wa Iran na njama za Washington za kukwamisha uhusiano wa pande mbili hizi hazitakuwa na natija yoyote.
Akizungumzia safari ya Dakta Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran huko Qatar na kuundika muundo mpya wa kidiplomasia wa kieneo amesema kuwa, sera za kieneo za Iran kama ilivyokuwa huko nyuma ambapo zimejengeka juu ya msingi wa uhalisia wa mambo.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia pia operesheni za kijeshi za Uturuki kaskazini mwa Syria na kusema kuwa, hakuna nchi yenye haki ya kufanya jambo lolote lile katika ardhi ya Syria bila ya idhini ya serikali ya Damascus.
Akizungumzia uungaji mkono wa Iran kwa usitishaji vita nchini Yemen, Bahram Qassemi amesema kuwa, tangu mwanzoni mwa mashambulio ya kijeshi ya Saudi Arabia na washirika wake huko Yemen, misimamo ya Tehran kuhusiana na kadhia hiyo ilikuwa wazi na bayana.