Qassemi: Iran ingali imefungamana na makubaliano ya nyuklia JCPOA
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekanusha uvumi kwamba Tehran imejiondoa katika makubaliano ya nyuklia yanayofahamika kwa kifupi kama JCPOA.
Bahram Qassemi amesema lengo la vyombo vya habari vinavyoeneza habari hizo za urongo ni kutaka kuibua mtafaruku na hali ya kuchanganyikiwa miongoni mwa wananchi wa Iran, huku akisisitiza kuwa taifa hili liko macho kutokana na njama na fitina za maadui.
Baadhi ya vyombo vya habari hususan vya Magharibi vimeripoti kuwa, Tehran imejiondoa kwenye makubaliano ya JCPOA, baada ya nchi za Ulaya kuchelewesha uzinduzi wa mfumo wa mabadilishano ya kifedha kati yazo na Iran.
Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akiwa safarini nchini India hivi karibuni alisema kuwa, "Nchi za Ulaya zinajitahidi kuhakikisha kuwa Iran inapata maslahi ya kiuchumi katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, lakini hazijaweza kuchukua hatua iliyotarajiwa. Tehran itaendelea kushirikiana na EU kuhusu mchakato wa kubuni Mfumo Maalumu kwa Ajili ya Mabadilishano ya Kifedha na Iran (SPV) lakini haitazisubiri milele."
Hata baada ya kuanza kutekelezwa awamu ya pili ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran mnamo tarehe 5 Novemba mwaka jana, hadi sasa Umoja wa Ulaya bado haujatekeleza mpango huo wa SPV.
Mei mwaka jana, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuitoa nchi yake katika makubaliano ya JCPOA, kwa lengo la kuyasambaratisha.