Rais Rouhani: Marekani na Uzayuni ndio chanzo kikuu cha ugaidi katika eneo
Rais Hassan Rouhani amesema: Chanzo kikuu cha ugaidi katika eneo la Mashariki ya Kati ni Marekani na Uzayuni; na kwa masikitiko, baadhi ya nchi za eneo zenye utajiri wa mafuta nazo pia zinawafadhili kifedha magaidi.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo mapema leo kabla ya kuondoka Tehran kuelekea mjini Sochi, Russia. Rais Rouhani ametoa mkono wa pole kufuatia kuuawa shahidi askari kadhaa wa jeshi la walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na akatuma salamu za rambirambi kwa familia za mashahidi hao, vikosi vya ulinzi, jeshi la walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi. Amesema: Jinai kama hizo zinazofanywa na watenda jinai waoga hazitaathiri kwa namna yoyote irada imara ya taifa kubwa la Iran; na taifa hili litaendelea kwa nguvu zote kufuata njia liliyoichagua.
Rais Rouhani amesisitiza kuwa, taifa la Iran halitosalimu amri katu kwa madola makubwa na akazihutubu baadhi ya nchi jirani ambazo ardhi zao zinatumiwa na makundi ya kigaidi kutekelezea hujuma zao za kigaidi kwa kusema: Tunawausia majirani watekeleze majukumu yao ya kisheria, ya kuishi kwa amani na kuwa na ujirani mwema na kutoyaruhusu makundi ya kigaidi yazitumie vibaya ardhi zao dhidi ya majirani zao.
Kuhusu kikao cha Sochi cha kujadili kadhia ya Syria, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Kulindwa umoja wa ardhi yote ya nchi hiyo ni jambo lenye umuhimu kwa Iran; na ardhi yote ya Syria inapasa iwe chini ya mamlaka ya serikali ya Damascus.
Rais Rouhani, ameondoka Tehran leo asubuhi kuelekea nchini Russia kufuatia mwaliko wa Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo wa kushiriki kikao cha marais wa nchi tatu za Iran, Uturuki, Russia kitakachofanyika mjini Sochi.
Pembeni ya kikao hicho, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran atakutana kwa ajili ya mazungumzo na kubadilishana mawazo na marais wa Russia na Uturuki.../