Feb 19, 2019 04:25 UTC
  • Iran yalaani hujuma ya kigaidi nchini Misri

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani hujuma ya kigaidi iliyolenga wanajeshi wa Misri katika eneo la Sinai.

Katika taarifa Jumatatu, Bahram Qassemi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alilaani hujuma hiyo ya kigaidi iliyotekelezwa na magaidi wa kundi la ISIS au Daesh. Qassemi sambamba na kutangaza kufungamana na familia za waathirika wa hujuma hiyo ya kigaidi amesisitiza kuwa: "Ugaidi ni tishio la pamoja la nchi za eneo na mapambano dhidi ya uovu huo yanahitaji azma ya kweli na jitihada za pamoja za nchi zote."

Katika hujuma ya kigaidi siku ya Jumamosi, magaidi wa kundi la ISIS au Daesh walihujumu kituo cha upekuzi cha jeshi la Misri huko Sinai ambapo afisa moja wa jeshi aliuawa na wengine 14 kujeruhiwa. Aidha taarifa  zinasema magaidi saba wa ISIS waliangamizwa.

Bahram Qassemi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran 

Mapigano kati ya askari usalama wa Misri na watu wenye silaha katika mkoa wa Sinai Kaskazini yalishika kasi mwaka 2014 tangu aingie madarakani huko Misri Rais Abdel Fattah al Sisi. Kundi la kigaidi linalojiita Wilaya ya Sinai ambalo ni tawi la kundi la kigaidi na ukufurishaji la ISIS nchini Misri linaendesha hujuma katika mkoa huo ambapo hadi sasa limeshaua mamia ya wanajeshi, maafisa wa polisi na raia wasio na hatia.

Tags