Bwabwaja mpya za Mike Pence dhidi ya Iran, kukaririwa tuhuma bandia
Marekani katika kipindi cha uongozi wa Rais Donald Trump, imeonyesha wazi misimamo yake ya kudhoofisha na kujaribu kuundoa madarakani mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran.
Katika uwanja huo, Trump sambamba na kutangaza kuiondoa nchi yake katika mapatano ya nyuklia maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, (JCPOA) na pia kufufua vikwazo vya nyuklia dhidi ya nchi hii, ameingia katika vita vya kiuchumi kwa lengo la kuibua umasikini na machafuko nchini Iran. Aidha katika uga wa kieneo, serikali ya Trump na katika fremu ya mpango wa stratijia ya usalama wa taifa ya mwaka 2017, alifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuunda miungano tofauti katika eneo la Mashariki ya Kati kwa lengo la kuifuta Jamhuri ya Kiislamu ya Iran au kuleta mabadiliko katika siasa za Tehran na hatua zake katika eneo. Wakati huo huo, serikali ya Washington imefanya njama nyingi na kushadidisha propaganda za vita dhidi ya Iran, ambapo katika uga huo viongozi wa ngazi za juu wa Marekani kila wanapopata fursa, wamekuwa wakitoa tuhuma tofauti dhidi ya Iran. Miongoni mwa viongozi hao ni Mike Pence, Makamu wa Rais wa nchi hiyo ambaye hivi karibuni amekariri madai bandia na yasiyo na msingi dhidi ya Tehran yakiwemo eti njama za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kutaka kuunda silaha za nyuklia na kuunga mkono ugaidi, na hivyo kuendeleza hatua za kiuhasama za Washington dhidi ya nchi hii.
Pence amedai kwamba Iran inajitahidi kuanzisha Holocaust nyingine na kusisitiza kwamba Washington itasimama imara ili kuizuia Tehran katika uwanja huo. Mike Pence ameyasema hayo akihutubia mkutano wa 'Harakati ya Kisiasa ya Wahafidhina' katika jimbo la Maryland, nchini Marekani na kudai kwamba uamuzi ya Trump wa kuiondoa nchi hiyo katika mapatano ya nyuklia ya Iran ulikuwa imara, huku akiyataja makubaliano hayo kuwa ni 'janga kubwa.' Pence amesema: "Rais Donald Trump kwa kutumia mamlaka aliyonayo katika uga wa kimataifa, aliamua kujiondoa katika mapatano hayo ya kimaafa na Iran ambayo yalikuwa ni tishio kubwa dhidi ya usalama na uthabiti katika eneo la Mashariki ya Kati na kwa Marekani pia." Hii ni katika hali ambayo kinyume na madai ya Pence, makubaliano ya nyuklia maarufu kama JCPOA, yalifikiwa baada ya muda mrefu wa mazungumzo mazito kati ya Tehran na kundi la 5+1. Aidha baada ya Marekani kujiondoka katika mapatano hayo, wajumbe wengine katika mapatano tajwa kupitia kundi la 4+1, wamekuwa na mtazamo unaopingana kikamilifu na Marekani. Russia, China na troika ya Ulaya, yaani Ujerumani, Ufaransa na Uingereza, kinyume kabisa na Marekani ambayo inadai kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijatekeleza makubaliano hayo na kwamba JCPOA sio makubaliano yenye taathira ya kuweza kusimamia miradi ya nyuklia ya nchi hii, zinaamini kwamba si tu kwamba Tehran imetekeleza ahadi zake zote katika fremu ya makubaliano hayo, bali imechangia pakubwa kufikiwa malengo ya makubaliano hayo kwa ajili ya kuzuia kutokea mizozo na migogoro katika ngazi ya eneo na kimataifa. Katika uwanja huo, Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ijumaa iliyopita na akitetea mapatano hayo ya JCPOA aliyataja kuwa yaliyopatikana baada ya juhudi za miaka 10 za makabiliano na mazungumzo na akamuhutubu pia Trump kwa kusema: "Kamwe hutapata makubaliano yaliyo bora zaidi ya hayo."
Kwa msingi huo na kinyume na matakwa ya Marekani na misimamo ya upande mmoja ya Washington ambayo daima imekuwa ikipiga ngoma ya kutaka kuyavunja na kushadidisha mashinikizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, madola makubwa duniani na hata washirika wakubwa wa Washington barani Ulaya wanasisitiza juu ya kulindwa mapatano hayo. Aidha madai mengine ya Makamu wa Rais wa Marekani dhidi ya Iran ni kwamba, eti Tehran inafanya njama za kuanzisha Holocaust nyingine katika eneo. Kuhusiana na suala hilo Pence amesema: "Iran na kwa namna ya wazi inataka kuibua Holocaust nyingine na iko katika njia ya kuitekeleza." Tunaweza kusema kuwa, Marekani inataka kujisahaulisha kwamba Wamagharibi, yaani Ujerumani ya Adolf Hitler ndio muhusika mkuu wa uanzishaji wa Holocaust, katika kipindi cha Vita vya Pili vya Dunia. Ni Wamaghari hao hao ndio baada ya kumalizika kwa Vita hivyo vya Pili nvya Dunia na kwa kisingizio cha kuuawa maelfu ya Mayahudi, waliwapeleka katika ardhi za Palestina na kisha kuwaundia utawala bandia wa Israel katika eneo. Aidha kwa kipindi cha miaka 70 sasa tangu utawala haramu wa Israel ulipoundwa Wamagharibi hao wamekuwa wakiunga mkono vita na hatua za ukandamizaji na ukatili mkubwa wa utawala huo dhidi ya Wapalestina na raia wa nchi jirani. Hii ni katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kuhusika na njama zozote za kufanya maangamizi dhidi ya Mayahudi kama ambavyo hata Mayahudi wanaoishi nchini Iran wanapewa haki kamili za uraia sambamba na kuwa na wawakilishi wao bungeni. Ni wazi kwa kila mtu kwamba Iran daima inapinga Uzayuni na vitendo vya kidhalimu vya utawala huo haramu dhidi ya Wapalestina na raia wa eneo la Mashariki ya Kati na kwamba njia pekee ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Palestina ni kufanyika kura ya maoni itakayowashirikisha raia asili wa Palestina kwa ajili ya kuainisha mustakbali wa taifa lao.